Sababu wanawake kuwa vinara wa mikopo

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza nchini, wanawake wanamiliki akaunti za mikopo ya kidijitali nyingi zaidi kuliko wanaume, jambo linalowafanya kuwa wakopaji wakuu katika sekta ya teknolojia ya fedha inayokua kwa kasi.

Takwimu mpya kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Ofisi za Taarifa za Wakopaji (Credit Reference Bureaus) zinaonesha idadi ya akaunti za mikopo ya kidijitali imepanda kutoka milioni 32.09 mwaka 2022 hadi kufikia milioni 193.33 mwaka 2024.

Katika kipindi hicho, akaunti za wanawake zimeongezeka kutoka milioni 11.3 hadi karibu milioni 120 na kwa mara ya kwanza kuwazidi wanaume.

Kwa sasa wanawake wanamiliki zaidi ya asilimia 60 ya akaunti za mikopo ya kidijitali nchini. Mwaka 2024 pekee, wanawake walikopa mikopo yenye thamani ya Sh152 bilioni sawa na asilimia 67 ya jumla ya mikopo yote kupitia mifumo ya kidijitali, ikiwazidi wanaume waliokopa Sh74 bilioni.

Thamani ya jumla ya mikopo iliongezeka kwa karibu asilimia 80 hadi kufikia Sh226.7 bilioni kufikia Desemba, 2024.

Kwa mujibu wa BoT, mikopo hiyo ni ya haraka inayotolewa moja kwa moja kama fedha za kielektroniki kwenye pochi za miamala ya simu za wateja.

Mikopo hiyo imewezeshwa kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya benki, taasisi za fedha ndogondogo na kampuni za simu za mkononi.

Sababu ya ongezeko kwa wanawake

Wachambuzi wanasema kupanda kwa kasi kwa mikopo ya kidijitali kwa wanawake kunatokana na ukweli kwamba, wanawake ni washiriki wakuu katika sekta isiyo rasmi nchini.

Wanajishughulisha na biashara za uuzaji wa vyakula (mama lishe), ushonaji na kilimo kidogo, ambavyo huhitaji mtaji wa mzunguko mara kwa mara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Usimamizi na Ujasiriamali (IMED), Dk Donath Olomi amesema mwenendo huo unaakisi uhalisia wa maisha.

“Wanawake tayari wanatawala sekta ya biashara ndogo na za kati (SME) nchini na ndio nguzo ya vikundi vya mikopo. Kinachotokea sasa kupitia mikopo ya kidijitali ni taswira hiyo hiyo kuhamia katika zama za kidijitali. Kwa kuwa mikopo hii inapatikana bila dhamana, imekuwa rahisi kwa wajasiriamali wanawake ambao mara nyingi hutengwa na mikopo rasmi,” amesema Dk Olomi.

Amesema kwa kupata fursa ya mikopo, wanawake wanaweza kukuza biashara zao, kusaidia familia na kuimarisha uhuru wao wa kiuchumi.

Hata hivyo, wachambuzi wanatahadharisha kuwa mikopo mingi inatumika kwa matumizi ya kawaida badala ya uwekezaji wa kuzalisha kipato, jambo linaloweza kuyumbisha kaya endapo tabia ya kukopa bila mpango itaendelea.

Dk Olomi amesema urahisi wa kupata mikopo unaweza kuwa na madhara.

“Riba ni kubwa, mara nyingine za kinyonyaji na urahisi wa kukopa kwa mikopo michache unawafanya wengi kukopa bila mpango sahihi wa kulipa. Ni rahisi sana kuchukua mkopo na kuutumia vibaya, ndipo msongo wa madeni unapojengeka,” amesema.

Mshauri wa kifedha na mtaalamu wa benki Kelvin Mkwawa, anakubaliana na tahadhari hiyo.

Amesema: “Upatikanaji wa mikopo ya kidijitali ni nguvu na udhaifu wake pia. Kwa upande mmoja, umefungua milango ya ujumuishaji wa kifedha, hasa kwa wanawake na vijana ambao awali hawakuwa na nafasi ya kupata mikopo. Lakini upande mwingine, urahisi huu unachochea watu kukopa kupita kiasi.”

 “Si jambo la nadra kumkuta mtu mmoja akiwa na mikopo kutoka kwa watoa huduma wengi wa kidijitali na pia vikundi vya kuweka na kukopa kwa wakati mmoja. Hii inaleta msongo wa kifedha, unakopa hapa ili kulipa kule.”

Mkwawa amesisitiza haja ya kuwepo kwa ulinzi zaidi wa wakopaji kwa sababu viwango vya riba na ada zilizofichwa, vinaweza kuwa vya juu mno na kuifanya gharama ya mkopo kuwa kubwa.

“Wakopaji wengi hawana uelewa wa kutosha au uwazi kuhusu wanachokubaliana. Tunahitaji mfumo madhubuti wa kusimamia mikopo hii ili isije ikawa mzigo kwa wananchi na uchumi,” amesema.

Pia, amehimiza benki, kampuni za fintech na wasimamizi kushirikiana kuweka viwango vya uwajibikaji katika utoaji mikopo sambamba na kukuza elimu ya fedha kwa wananchi ili waelewe hatari za kukopa.

Juhudi za udhibiti, ujumuishaji wa kifedha

Wadau wa ulinzi wa wateja wanakubaliana kuwa kuna haja ya kuwepo kwa ulinzi thabiti zaidi ili kuzuia unyonyaji.

Uwazi wa gharama, kuweka kikomo cha ada za kinyonyaji na usimamizi bora wa matumizi ya taarifa binafsi, ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele.

Kwa mujibu wa BoT, jumla ya benki na taasisi za kifedha sita zilikuwa zikitoa huduma za mikopo ya kidijitali kupitia ushirikiano na kampuni za simu za mkononi. Ushirikiano huu umeimarisha kwa kiasi kikubwa ujumuishaji wa kifedha nchini kwa kuongeza upatikanaji wa mikopo.

Ongezeko hilo pia limechangiwa na kuimarika kwa upatikanaji wa intaneti, uliopanda hadi zaidi ya asilimia 90 na kuruhusu watu wengi zaidi, wakiwamo wale wa maeneo ya vijijini, kuomba na kupata mikopo ya kidijitali.