Salum Mwalimu aahidi Tanzania ya ‘maziwa na asali’

Tanga. Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amewaomba Watanzania kumchagua kwa kishindo ifikapo Jumatano Oktoba 29, 2025, ili alitengeze taifa lenye ustawi na neema, akiahidi kuigeuza Tanzania kuwa “nchi ya maziwa na asali’ iwapo atapewa ridhaa ya kuingia Ikulu.

Akihutubia wakazi wa Muheza katika viwanja vya Madaba, jijini Tanga kwenye mkutano wa kwanza wa kampeni za chama hicho, tangu kuzinduliwa rasmi jana Jumapili jijini Dar es Salaam, Mwalimu amesema serikali ya Chaumma itaweka kipaumbele katika kuondoa umaskini, kuongeza ajira kwa vijana na kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.

“Kikubwa nawaomba wekeni imani kwangu, imani huzaa imani, msiniangalie kwa umri wangu, au umbile langu, nipimeni kwa dhamira niliyonayo katika uadilifu na utendaji katika kwenda kulitumikia Taifa hili, kama umri ni kigezo, basi miaka 60 nchi hii tuliwakabidhi wazee, Marais wote wametoka CCM, kama uongozi ni umri, Muheza msingelia maji.

“Kama uongozi ni umri, msingelia shida ya kilimo, natambua shida mlizonazo, si za bahati mbaya ila zinatokana na kuikumbatia CCM, sioni aibu kuwaambia matatizo mliyonayo hayajasababishwa na Mungu, wala jirani yako bali ni CCM,” amesema Mwalimu.

Amesema Muheza imejaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba nzuri katika milima yote inayozunguka eneo hilo lakini, pamoja na neema hiyo, wanaweza kumuuliza Mungu wamekosea jambo gani.

“Nichagueni niende Ikulu nikaangalie nini kinashindakana watu kupata maendeleo katika nchi hii, achaneni na wazee, nichagueni Mwalimu kama mnahitaji maziwa na asali yatoke kwenye mabomba yenu,” amesema Mwalimu.

Amesema wananchi wanapaswa kukubaliana kwamba mwaka huu uwe wa ‘masela’ waende Ikulu wakaangalie kuna shida gani inayosababisha wakose maendeleo, huku akisema yeye ameshajitolea kuwaongoza Watanzania.

“Tukaangalie nini kinasababisha vijana wasipate ajira, nini kinasababisha wanawake waende kupata huduma kwa shida, wanaenda kujifungua wamebeba vifaa kama wanaenda kuanza kidato cha kwanza,” amesema mgombea huyo.

Ahadi kwa wakazi wa Muheza

Mwalimu amesema akiingia madarakani kwanza serikali watakayoiunda itawasambazia huduma ya majisafi na salama, ili kuondoa changamoto hiyo inayolalamikiwa kwa muda mrefu licha ya nchi kuwa na vyanzo vingi vya maji.

“Pia tutawekeza kwenye sekta ya kilimo kusudi  mkifanye kwa tija, tunataka kujenga viwanda vya kuchakata matunda watu wapate juisi,” ameahidi na kuongeza;

 “Watanzania wakiamua leo, nchi hii inaweza kuwa paradiso. Mnachotakiwa kufanya ni uamuzi sahihi. Kama mnataka nchi ya maziwa na asali, basi chagueni Salum Mwalimu, chagueni Chaumma,” amesisitiza.

Mwalimu amezungumzia pia mpango wa chama chake ni kujenga uchumi jumuishi unaotegemea kilimo cha kisasa, viwanda vya ndani na matumizi bora ya rasilimali za taifa kama gesi, madini na ardhi.

Pia, amekosoa mfumo wa sasa wa kiuchumi akidai unawanufaisha wachache huku wananchi wengi wakiendelea kubaki katika umasikini.

Akizungumza baada ya kutambulishwa, mgombea ubunge wa Jimbo la Muheza kupitia Chaumma, Yosepha Komba;

“Yosepha Komba si mgeni, mlimfahamu tangu akigombea kupitia chama fulani, kwa sasa nimekuwa ‘Simba’ baada ya kuhama pori, naomba mridhie kunipokea na kuniunga mkono niwe mbunge wenu.”

Amesema Muhenza inachangamoto ya maji, anatakiwa kuitatua ili ifikie mwisho kwa kuwa kila kona kuna vyanzo vya maji.

Chaumma kinataka kuwasaidia wanawake  wanaopitia wakati mgumu kwa kuyatafuta maji maeneo ya mbali.

(Vyama vingine vimeshindwa kutatua kero hii, wananchi nawaomba mchagueni mgombea uris wa Chaumma, wabunge na madiwani tukaikomeshe changamoto hii,” amesema Komba.