Serikali yakata mishahara ya wabunge kutuliza waandamanaji

Jakarta. Rais wa Indonesia, Prabowo Subianto, ametangaza kupunguza mishahara na baadhi ya marupurupu kwa wanasiasa wa taifa hilo, ikiwemo wabunge, ili kutuliza maandamano yanayoendelea nchini humo.

Hatua hiyo inakuja kutokana na maandamano ya wiki kadhaa katika taifa hilo la Kusini-Mashariki mwa Asia, ukiwemo mji mkuu, Jakarta, ulioshuhudia mamia ya waandamanaji wanaoipinga serikali.

Maandamano hayo yamesababisha mapigano kati ya waandamanaji na polisi na kusababisha vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa miundombinu, ikiwemo maduka, barabara, na ofisi za taasisi za kiserikali.

Kwa sehemu kubwa, maandamano hayo yamechochewa na kupanda kwa posho ya wabunge kila mwezi na kifo cha dereva aliyekuwa akipewa huduma, kilichosababishwa na kupigwa na askari.

Akitoa taarifa ya kupunguzwa kwa posho hizo siku ya Jumapili, Rais Subianto amesema marupurupu mengi yataondolewa na posho ambazo awali hazikuwepo, na kuwataka wabunge na wanasiasa kuipokea hali hiyo.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo pia ameahirisha safari ya kwenda China kutokana na machafuko hayo.

Amesema maandamano hayo, yasipodhibitiwa, yatakwenda kuwa uhaini na ugaidi kutokana na uwepo wa watu ambao pia wanatumia nafasi hiyo kufanya uporaji.

“Maandamano yamekwenda zaidi katika baadhi ya miji, na kinachoonekana ni kuwa amani inaweza kutoweka kabisa na kusababisha ugaidi na uhaini,” amesema Subianto.

Kiongozi huyo pia amewaagiza polisi na vikosi vya jeshi kuchukua hatua kali dhidi ya uporaji na uharibifu wa mali unaofanywa na waandamanaji.

Hata hivyo, waandamanaji bado hawajaridhishwa na hatua hiyo, wakiitaka serikali kuendelea kuchukua hatua zaidi ikiwa inataka waandamanaji watulie.

Muzammil Ihsan, mkuu wa Bodi ya Watendaji Wote wa Wanafunzi wa Indonesia, kundi kubwa la wanafunzi nchini humo, amesema maandamano yataendelea kupewa kipaumbele zaidi katika kipindi hiki hadi serikali itakapojirekebisha zaidi.

“Serikali lazima isuluhishe matatizo yaliyokita mizizi, kwa vijana na kila lililopo mtaani, kupunguza mishahara ya juu na kupambana na ufisadi,” amesema Ihsan.

Maandamano hayo pia yameonekana kuwa mtihani wa kwanza muhimu kwa uongozi wa Prabowo tangu ashike urais Oktoba mwaka jana.

Jenerali wa zamani ambaye amekuwa akizuiliwa kupata nafasi hiyo kwa miongo kadhaa kwa madai ya ukiukaji wa haki za binadamu, na wakosoaji wake wameelezea wasiwasi wa Indonesia kurejea katika hali yake ya kimabavu, licha ya yeye kuahidi kuongoza kwa kufuata sheria.

Elidaima Mangela (UDOM), kwa msaada wa Mashirika ya Habari