Siku 30 za ahueni ukisalimisha silaha haramu kwa hiyari yako

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetangaza msamaha wa kutoshitakiwa kwa wamiliki wa silaha haramu watakaosalimisha silaha kwa hiyari kuanzia leo Septemba 1, 2025 hadi Oktoba 31, 2025.

Msamaha huo umetolewa chini ya mamlaka ya Kifungu cha 66 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya mwaka 2015, Sura ya 223 na marejeo ya mwaka 2023, kupitia Tangazo la Serikali Na. 537 la Agosti 29, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, iliyotolewa leo Jumatatu, Septemba 1, 2025,  hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya kimataifa na kikanda kuhusu udhibiti wa silaha ndogo na nyepesi, ambazo mara nyingi zimekuwa chanzo cha uvunjifu wa amani, hofu, majeruhi na vifo.

“Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, inatekeleza maazimio ya mikutano ya kimataifa ikiwemo ule wa Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa wa Julai 2018 na ule wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, Julai 2017, ambapo ilikubaliwa Septemba iwe mwezi wa usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari hadi mwaka 2030.

“Kwa mujibu wa masharti ya msamaha huu, usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari utafanyika nchi nzima kuanzia leo Septemba 1 hadi Oktoba 31, 2025. Silaha zitakazokabidhiwa zitasalimishwa katika kituo chochote cha Polisi nchini, Ofisi ya Serikali za Mitaa au kwa Mtendaji Kata/Shehia kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Imeongeza kuwa mtu yeyote atakayesalimisha silaha katika kipindi tajwa hatowajibishwa kwa hatua zozote za kisheria, lakini yeyote atakayekutwa na silaha baada ya muda wa msamaha kumalizika atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

“Wananchi wanahimizwa kutumia fursa hii kusalimisha silaha haramu, ikiwemo zile zilizokuwa zikimilikiwa kihalali na ndugu waliokwishafariki dunia.

Aidha, kampuni binafsi za ulinzi haziruhusiwi kuazimisha au kurithisha silaha kinyume na taratibu; na endapo kuna silaha zinazotumika kinyume cha sheria zirejeshwe kwa wamiliki halali au zisalimishwe kwenye vituo vya Polisi katika kipindi hiki cha msamaha,” imeeleza taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Serikali imeziagiza kampuni za ulinzi ambazo zimesitisha huduma zao kurejesha silaha zote walizokuwa wanamiliki kihalali ili kuepuka matumizi yasiyo sahihi.

“Wamiliki wa silaha halali pia wanatakiwa kuzingatia matumizi sahihi na utunzaji bora wa silaha kwa mujibu wa sheria, vinginevyo leseni zao zinaweza kufutwa na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.