KIKOSI cha Simba kinarudi tena katika kambi ya mazoezi kuanzia leo Jumatatu, ikiwa ni saa chache tangu irejee kutoka kambini jijini Cairo, Misri ilikokuwa kwa muda wa mwezi mmoja ikijifua na kucheza mechi nne za kirafiki za kimataifa za kujipima nguvu.
Simba ilianza kambi ya muda mfupi jijini Dar es Salaam kisha Julai 30 ikasafiri hadi Ismailia, Misri na kukaa kwa muda wa wiki mbili kabla ya kuhamia Cairo ambako iliifunga kambi hiyo Alhamisi iliyopita kabla ya kurejea nchini na kuwapa mastaa wa timu hiyo mapumziko mafupi.
Taarifa kutoka ndani ya Simba ni kwamba mastaa wa timu hiyo wanatarajiwa kuanza mazoezi na kambi mpya kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, kujiandaa na tamasha la Simba Day litakalofanyika Septemba 10 kisha kucheza mechi ya Ngao ya Jamii siku sita baadaye dhidi ya Yanga.
Mara baada ya mechi hiyo ya Ngao itakayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba itasafiri hadi Gaborone, Botswana kwa ajili ya mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao, Gaborone United.
Kwa hesabu zilivyo ni kwamba, kikosi cha Simba hakina muda wa kulala kuanzia sasa hadi mechi hiyo ya kwanza ya Botswana, kwani itarudi kucheza mechi ya Ligi Kuu ya msimu wa 2025-26 dhidi ya Fountain Gate Septemba 25 na siku nne baadaye itarudiana na Gaborone United.
Ukipiga hesabu za haraka ni kwamba kwa muda wa mwezi mzima huu wa Septemba, Simba itakuwa bize na mechi mechi tano, zikijumisha nne za mashindano ikiwamo Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi kama hiyo kwa msimu uliopita.
Simba ilifungwa na Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii kwa bao 1-0, kisha ilifunga msimu wa 2024-25 kwa kulala tena mbele ya Yanga kwa mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara, kitu ambacho Wanamsimbazi hawataki kuona kinatokea tena Septemba 16.
Mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone zitakazopigwa kati ya Septemba 20-28 ni mtihani mwingine wa kikosi cha Fadlu Davids, kwani tofauti na misimu kadhaa timu hiyo ikianzia raundi ya pili, safari hii imeanza raundi ya kwanza, licha ya msimu uliopita kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco.
Pia hata mechi ya kwanza ya Ligi Kuu itakayopigwa Septemba 25, siku chache kabla ya kumalizana na Gaborone United, ni mtihani mwingine kwa kikosi hicho kilichomaliza nafasi ya pili katika Ligi ya msimu uliopita, ikifikisha misimu minne mfululizo bila ya taji la Ligi na Kombe la Shirikisho.
Mapema kocha wa Simba, Fadlu Davids aliyekuwa amepitia Afrika Kusini kwa dharura na inayodaiwa amesharejea, alikaririwa na Mwanaspoti akisema kwamba, msimu huu kwa aina ya kikosi alichonacho ana imani ya kufanya makubwa kwa michuano ya ndani na ya kimataifa.
“Tuna nafasi ya kufanya makubwa kwa msimu ujao. Tunajua kiu ya kila shabiki na mpenzi wa Simba ni kutaka kuona tunafika mbali zaidi ya tulichofanya msimu uliopita. Nafasi hiyo tunayo kwa kambi tuliyoifanya Misri na hata aina ya kikosi kilichopo. Tunajipanga,” alisema Fadlu.
Katika dirisha la usajili linalotarajiwa kufungwa wiki ijayo, Simba imesajili wachezaji zaidi ya 10 wakiwamo sita wa kigeni, Neo Maema, Mohammed Bajaber, Naby Camara, Jonathan Sowah, Rushine de Reuck na Alassane Kante.
Kwa wazawa Simba imewanasa Seleman Mwalimu ‘Gomes’, Anthony Mligo, Charles Semfuko, Morice Abraham, Wilson Nangu na Yakoub Suleiman, huku ikimpandisha pia Hussein Idd.
v Fountain Gate (Ligi Kuu)