Zanzibar. Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikiweka nguvu katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, wadau wa sekta hiyo wameshauri kuongezwa jitihada zaidi ili wananchi wapate nishati mbadala kwa haraka, wepesi na gharama nafuu.
Msingi wa ushauri huo unatokana na hali ya sasa ambapo wananchi wengi bado wanategemea kuni na mkaa wa miti, kutokana na upatikanaji wake kwa urahisi na gharama ndogo ikilinganishwa na nishati safi, ambayo bado haijafikia kiwango cha kuridhisha.
Serikali inasisitiza kuwa ipo kwenye hatua madhubuti za utekelezaji wa sera mpya ya nishati ya mwaka 2025, pamoja na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa Tanzania wa mwaka 2024–2034. Lengo ni kuondoa utegemezi wa nishati chafu, ambazo zinachangia uharibifu wa mazingira na athari za kiafya kwa wananchi, ikisisitiza kushirikisha wadau na kutoa elimu ili kufanikisha malengo hayo.
Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shaib Hassan Kaduara, anasema SMZ imeingia makubaliano na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kwa ajili ya kuingiza mkaa safi wa kupikia, ili kuwawezesha wananchi kupata nishati mbadala kwa gharama nafuu.
“Tumeamua bei inayopatikana kule Bara iwe ile ile itakayotumika Zanzibar. Tayari mpango huo umeanza kutekelezwa, ingawa bado hatujaona matokeo ya moja kwa moja kwa sababu hii ni teknolojia mpya kwa visiwa vyetu,” anasema Kaduara.
Waziri huyo anaeleza kuwa matumizi ya mkaa mbadala ni nafuu zaidi ikilinganishwa na mkaa wa miti.
“Kwa Zanzibar ni teknolojia mpya, kwa hiyo tunaendelea kuwashawishi wananchi na kufanya mobilization ya teknolojia hiyo ili waielewe zaidi. Mkaa wa Sh1,000 unatosha kupika chakula cha familia ya watu watano. Utaona namna gani, iwapo tukiingia huko moja kwa moja, bei yake ni rahisi na wananchi wengi wataweza kumudu gharama hizo,” anasema.
Kwa upande wa gesi, Waziri Kaduara anasema juhudi zimeanza kuzaa matunda na bei zimeanza kushuka. “Kwa sasa Serikali tayari inafanya kazi ya kujaza gesi hapa Zanzibar. Kupitia Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Maji (Zura), tupo mbioni kuweka bei elekezi kwa ajili ya matumizi ya gesi,” anasema.
Anaongeza kuwa Serikali inafanya jitihada mbalimbali, ikiwemo kuweka punguzo, kuwapatia wananchi mitungi ya gesi bure, pamoja na kuondoa kodi kwa vifaa vya madini vinavyotumika kwenye sekta hiyo.
“Kwa sasa tumepanga na kuratibu bei za gesi, ambapo mtungi wa kilo tatu unauzwa kati ya Sh12,000, kilo sita kati ya Sh20,000 na Sh25,000, kilo 15 kati ya Sh50,000 na Sh60,000, na kilo 38 kati ya Sh120,000 na Sh150,000,” anasema.
Vilevile, anasema wizara yake imeendelea kutoa mafunzo ya matumizi bora ya nishati safi kwa wanafunzi na walimu wa shule mbalimbali Unguja na Pemba.
“Mpaka sasa shule nane zimepatiwa mafunzo hayo, na tumeweka mpango wa kuyapanua kwa masheha, wilaya, mikoa, na taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi,” anasema.
Katika hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26, kiwango cha gesi kilichoingizwa nchini kati ya Julai 2024 na Machi 2025 kilikuwa kilo 8.59 milioni, huku matumizi yakifikia kilo 9.26 milioni, ikidhihirisha ukubwa wa mahitaji.
“Serikali italipa kipaumbele suala la mahitaji ya nishati kwa wanawake, hususan kwa matumizi ya nishati safi nyumbani, biashara ndogo ndogo na huduma muhimu za jamii kama shule na vituo vya afya,” anasema Kaduara.
Kupitia mradi wa ZESTA unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, Serikali imesema itatoa kipaumbele kwa kaya maskini zinazoongozwa na wanawake wa kipato cha chini, ili kuhakikisha zinapata umeme na nishati mbadala kwa urahisi.
“Kuna mpango kwa ajili ya wanawake (Clean Cooking Strategy) unaolenga kuwarahisishia shughuli zao za kila siku na kupunguza athari zitokanazo na matumizi ya kuni na mkaa,” anasema.
Pamoja na jitihada hizo za Serikali, bado wananchi wanakiri changamoto za upatikanaji wa nishati safi.
Khamis Bakari Njokepa, kijana aliyekuja na ubunifu wa kutengeneza majiko ya mkaa wa kawaida, anasema wanaendelea na kazi hiyo kwa sababu bado kuna mahitaji makubwa ya mkaa wa miti.
“Sisi hapa tunatengeneza majiko haya kwa sababu bado kuna mahitaji makubwa. Wananchi wengi wanatumia mkaa wa miti kwa sababu bado hakujawa na matumizi ya mkaa mbadala kwa kiwango cha kutosheleza. Tunategemea Serikali itatoa msaada wa nishati mbadala kama makaa ya mawe au mkaa wa viwandani ili tuone namna ya kusaidia,” anasema Khamis.
Anaongeza kuwa, “Sio kwamba tunapenda. Tunajua matumizi ya mkaa wa miti unasababisha miti kuisha, lakini kwa kuwa hakuna mbadala wa kutosha, ndio maana wananchi wanaendelea kutumia. Kama Serikali itasikia katika nishati safi, tupo tayari kuendana na mabadiliko hayo.”
Kwa siku, Khamis hutengeneza majiko 20 hadi 25 na kuyauza kati ya Sh7,000 na Sh250,000, kutegemea ukubwa na malighafi zilizotumika.
“Najivunia kujiajiri na kuanzisha ajira ndogo ndogo kwa vijana wengine, kwani inasaidia kupata kipato cha kuendesha familia na kuwasaidia wenzangu,” anasema, na kubainisha wamejiajiri vijana watano.
Ussi Haji Abubakar, muuzaji wa mkaa eneo la Kwa Mabata – Unguja, anasema bado elimu ya matumizi ya mkaa mbadala ni ndogo na hata upatikanaji wake unakabiliwa na changamoto.
“Wakati mwingine sio kwamba watu hawataki kutumia nishati safi, lakini kuna tatizo la upatikanaji. Unaposhindwa kupata mbadala kwa urahisi, wananchi hulazimika kurudi tena kwenye mkaa wa miti,” anasema.
Mdau wa mazingira, Hashim Mbaraka Hamad, anasema bado elimu ya matumizi ya nishati safi haijawa ya kutosha na changamoto ya upatikanaji inaendelea.
“Nishati ina matumizi mengi, lakini tukizungumzia kupikia, hapa ndipo tunapomgusa kila mmoja wetu. Kwa Watanzania zaidi ya milioni 61 hakuna asiyekula, na asilimia kubwa ya hawa bado wanatumia nishati chafu kwa sababu ni rahisi na inapatikana kwa haraka,” anasema.
Anaongeza kuwa, “Ukienda vijijini, wengi hawatumii gharama kutafuta kuni. Sasa inapokuja mpango huu ili kufanikiwa, lazima nishati mbadala ipatikane kwa wingi na kwa bei nafuu. Serikali ikiongeza mkakati wa kushusha gharama za gesi na kurahisisha uingizaji wa mkaa mbadala, ndipo wananchi wataweza kubadilika.”
Kwa sasa, Serikali na wadau wameanza kuchukua hatua kuelekea kupunguza utegemezi wa nishati chafu. Hata hivyo, changamoto kubwa zinazobaki ni upatikanaji wa nishati safi kwa uhakika na uwezo wa wananchi wengi kumudu gharama.
Ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, wabunifu na wananchi unaonekana kuwa nguzo muhimu ya kuhakikisha mabadiliko hayo yanafanikiwa kwa faida ya vizazi vijavyo.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.