Tanzania Prisons yamnyatia Chilunda | Mwanaspoti

WAKATI KMC ikielezwa huenda ikaachana na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Shaaban Idd Chilunda, uongozi wa Tanzania Prisons upo katika mazungumzo na kambi ya mchezaji huyo, ili kuipata saini yake kwa msimu ujao wa 2025-26.

Chilunda ni miongoni mwa nyota wanaotajwa huenda wakaachana na KMC kutokana na kutofikia makubaliano ya kusaini dili jipya, jambo linaloziingiza vitani timu mbalimbali zinazoonyesha nia ya kumuhitaji, huku Prisons ikiwa mstari wa mbele.

Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa Prisons, kimeliambia Mwanaspoti hadi sasa mazungumzo yanaendelea baina ya pande zote mbili kwa ajili ya kumsajili nyota huyo, ingawa hakuna makubaliano yaliyofikiwa hadi sasa japo kuna mwanga huko mbele.

“Hakuna makubaliano rasmi baina ya pande zote mbili yaliyofikiwa, japo ni kweli mazungumzo hayo yapo na yanaendelea pia vizuri, tumedhamiria kufanya maboresho makubwa kwa lengo la kuongeza ushindani wa kikosi chetu,” kilisema chanzo hicho.

Chilunda mbali na kuichezea KMC, aliwika na Azam FC na Simba pia akiwahi kukipiga CD Tenerife na CD Izarra za Hispania na Moghreb Atletico Tetouan ya Morocco, jambo linaloivutia Prisons kutokana na uzoefu wake mkubwa.

Kwa msimu wa 2024-25, mshambuliaji huyo alifunga mabao mawili ya Ligi Kuu Bara, yote katika ushindi wa KMC wa mabao 3-2 dhidi ya Prisons, kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge Dar es Salaam, Aprili 2, 2025.