Tetemeko laua 250, likijeruhi 500 Afghanistan

Watu 250 wamefariki na wengine 500 wamejeruhiwa baada ya kutokea tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa Richer scale 6.0 nchini Afghanistan usiku wa kuamkia leo.

Tukio hili linajiri takriban miaka miwili baada ya tetemeko jingine kubwa lililoua zaidi ya watu 1,000 katika Mkoa wa Herat mwaka 2023 na kuacha  hatari kubwa ya majanga ya asili kulikumba taifa hilo.

Al Jazeera imeripoti kuwa, tetemeko hilo lilitikisa majimbo ya Kunar na Nangahar yaliopo upande wa Mashariki mwa taifa hilo saa sita  usiku wa Jumatatu, lakini pia lisambaa hadi baadhi ya maeneo ya Taifa la Pakistan.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari ya Afghanistan inaeleza kuwa, watu 250 wamefariki na wengine 500 wamejeruhiwa katika tetemeko hilo lenye ukubwa wa Richer Scale 6.0.

Imeelezwa kuwa, tetemeko hilo lilianzia Mji wa Jalalabad Alalabad katika Jimbo la Nangahar likiwa na kina cha kilomita nane na baadaye lilifika katika  wilaya za Nur Gal, Sawki, Watpur, Manogi na Chapa Dara za Mkoa wa Kunar na maafa yakatokea.

“Kitovu cha tetemeko hilo kilirekodiwa katika Jimbo la  Nangahar. Vijiji vyote vya Jimbo la Kunar vimeathirika vibaya, serikali imetuma timu za dharura kutoka Kabul na mikoa ya karibu ili kusimamia shughuli za ukoaji,” inaeleza taarifa hiyo.

Wizara hiyo pia imeweka wazi kuwa, athari za tetemeko hilo zinaweza kuongezeka kwa kuwa, limetokea majira ya usiku wakati watu wengi wakiwa kwenye makazi yao katika eneo hilo.

Profesa wa Sayansi ya Sayari kutoka chuo cha Curtin Chris Elders, amesema kinachosababisha serikali kutarajia athari  kubwa zaidi katika tetemeko hilo ni maporomoko ya udongo na miamba iliyopo jirani na eneo hilo.

Elidaima Mangela kwa msaada wa Mashirika ya habari