Times FM Kutangaza Mubashara Kagame Cup, Kuanza Kesho – Global Publishers

MSIMU mpya wa Kombe la Kagame (Kagame Cup) unaanza kesho Septemba 2, 2025 kwa mechi mbili kuchezwa kwenye uwanja wa Major General Isamuhyo, Dar es Salaam, mechi hizo zikitarajiwa kutangazwa mubashara na kituo cha radio cha Times FM.

Times FM imeingia ubia na Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati ( Cecafa) kutangaza mashindano hayo yanayoanza Septemba 2-15 jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Masoko na mawasiliano wa Cecafa, Andrew Jackson Oryada amesema wameingia ubia na Times FM ambayo itatangaza mubashara mechi zote.

“Tunafuraha kubwa kuwa mshirika na Times FM, kituo pekee cha radio kinachotangaza michezo hapa nchini Tanzania, tunaamini ushirikiano huu utaongeza kwa kiwango kikubwa mwonekano na usikivu wa Mashindano ya CECAFA Kagame Cup 2025,” alisema.

Alisema kupitia ushirikiano huo, Times FM itatoa matangazo ya kipekee na ya kina ya mashindano ya Kagame Cup, yakiwemo mahojiano na makocha pamoja na manahodha wa timu, matukio ya nyuma ya pazia wakati wa mazoezi, taarifa kutoka vyumba vya kubadilishia, na maudhui ya mchezaji bora wa mechi.

Mashindano haya yatashirikisha timu kutoka Tanzania, Zanzibar, Kenya, Rwanda, Burundi, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Djibouti na Ethiopia.

Mchambuzi wa michezo wa Times FM, Emmanuel Ndalama alisema mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Septemba 2 hadi 15 yatafuatiliwa moja kwa moja kupitia kituo cha Times FM kama redio mshirika.

“Wasikilizaji kote nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wataweza kufuatilia matangazo ya moja kwa moja, mahojiano ya kipekee, uchambuzi wa kina na maoni ya moja kwa moja kutoka viwanjani.

“Kwa ubia huu, Times FM imeandika historia kama redio pekee ya michezo inayorusha matangazo masaa 24.
Nyota na nahodha wa zamani wa Yanga, Juma Abdul ambaye ni miongoni mwa wachambuzi wa mashindano hayo kupitia radio ya Times FM alisema ni mashindano ambayo yanakwenda kuongeza ushindani na kuonyesha vipaji vipya, akimtolea mfano nyota wa zamani wa timu hiyo, Didier Kavumbagu ambaye alisajiliwa baada ya kuonekana kwenye Kagame Cup.

Bingwa wa msimu huu ataondoka na medali ya dhahabu, kombe na kitita cha dola 30,000, mshindi wa pili medali ya fedha na dola 20,000 wakati mshindi wa tatu atapewa dola 10,000 na medali ya shaba.
Caption.

Mkuu wa Masoko na mawasiliano wa Cecafa, Andrew Jackson Oryada (kushoto) akizungumza wakati wa kutangaza ushirikiano na kituo cha redio cha michezo cha Times FM. Kulia ni mchambuzi wa Times FC na mchezaji wa zamani wa Yanga, Juma Abdul. Kushoto ni mchambuzi wa michezo, Emmanuel Ndalama.