Wabrazili wakoleza mzuka Mlandege | Mwanaspoti

KOCHA Mkuu wa Mlandege inayojiandaa na mechi za Kombe la Kagame 2025 na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Hassan Ramadhan Hamis amesema amefurahia kutua kwa nyota wanne wa kigeni kutoka nchi tofauti wakiwemo Wabrazili wawili, huku akiahidi kufanya vizuri kimataifa.

Mlandege imewanasa beki wa kati Davi Nasciimento na kiungo mkabaji Vitor De Souza raia wa Brazil, Hamis M’sa wa Comoro na winga Mghana, Ishmael Robono walioanza kujifua na wenzao kwa maandalizi ya Kombe la Kagame 2025 yanayoanza kesho na yale ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Hamis alisema ongezeko la nyota hao ni sehemu ya ahadi ya uongozi kushusha mashine mpya akiamini timu itakuwa sehemu nzuri ya kuonyesha ushindani kimataifa na ligi ya ndani.

“Ni kweli nyota hao wamejiunga na timu yetu na tayari wameanza kuonyesha ushindani mazoezini, tunaamini ujio wao utakuwa chachu ya mafanikio msimu huu, ambapo lengo ni kufikia malengo ya kucheza hatua ya makundi kimataifa na kutetea taji la ndani,” alisema Hamis na kuongeza;

“Maendeleo kwa ujumla timu yetu inaendelea poa na tunatarajia kutumia michuano ya Kagame tukiwa Kundi B pamoja na KMC, Bumamuru na APR tutayatumia mashindano hayo kama sehemu ya maandalizi ya msimu sambamba na michuano ya kimataifa.”

Hamis akizungumzia maandalizi kwa ujumla alisema yanaenda vizuri na wachezaji wanaonyesha na uhitaji wa kuiwakilisha vizuri nembo ya Mlandege katika michuano ya ndani na kimataifa.

“Unajua Zanzibar timu zetu hazina rekodi nzuri kimataifa zimekuwa zikitolewa hatua za mwanzo, sasa tunataka kuondoka kwenye nafasi hiyo ambayo sio nzuri na ndio maana timu imefanya usajili mzuri lengo ni kuweka rekodi nzuri,” alisema kocha huyo ambaye timu hiyo itaanza mechi za raundi ya kwanza za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuvaana na Insurance ya Ethiopia.

Timu itakayoibuka mbabe katika mechi hizo zitakazopigwa kati ya Septemba 19-28 itavaana na mshindi kati ya APR ya Rwanda na watetezi wa taji hilo, Pyramids ya Misri.

Katika michuano ya Kombe la Kagame, Mlandege imepangwa kukata utepe kesho Jumanne dhidi ya KMC kabla ya Septemba 5 kumenyana na APR ya Rwanda na kumalizia makundi kwa kuumana na Bumamuru ya Burundi Septemba 8.