Wacolombia Azam FC wajiandaa kutua KMC

MABOSI wa KMC FC wako katika mazungumzo ya kukamilisha usajili wa nyota wawili wa Azam FC Wacolombia, kiungo, Ever Meza na mshambuliaji wa timu hiyo, Jhonier Blanco ambao wamekuwa pia hawana wakati mzuri tangu walipojiunga na kikosi hicho.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Azam inaweza kuwatoa nyota hao kutokana na kuwa na nafasi finyu ya kucheza ndani ya kikosi hicho, huku uongozi wa KMC ukiamini unaweza kuwapata kwa mkopo kwa sababu ya ushirikiano wao.

“Mazungumzo baina ya pande zote mbili yanaendelea na yanaweza yakakamilika ikiwa kila kitu kitaenda sawa, tunaamini kwa uwezo wao watakuwa msaada mkubwa kwetu kwa msimu huu wa 2025-26, hivyo acha tuone itavyokuwa,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kimeliambia Mwanaspoti, wachezaji hao wamependekezwa na Kocha wa KMC, Mbrazil Marcio Maximo anayewataka ili wakaongeze nguvu ndani ya timu hiyo kwa kushirikiana na waliopo, akiamini pia wataleta tija kutokana na uzoefu walionao.

Timu hizo zimekuwa na uhusiano mzuri kwani hata msimu wa 2024-25, mabosi wa Azam walimpeleka aliyekuwa kipa wa kikosi hicho mzaliwa wa Ufaransa, anachezea timu ya taifa ya Comoro, Ali Ahamada, jambo linaloweza kutokea pia kwa Wacolombia.

Meza aliyezaliwa Julai 21, 2000, alijiunga na Azam Julai 1, 2024, akitokea Alianza FC aliyokuwa anaitumikia kwa mkopo kutoka Leonnes FC zote za kwao Colombia, ambapo alisaini mkataba wa miaka minne na kikosi hicho hadi mwaka 2028.

Blanco aliyezaliwa Oktoba 18, 2000, alijiunga na Azam Julai 1, 2024, akitokea Klabu ya Aguilas Doradas ya mji wa Rionegro, inayoshiriki Ligi Kuu ya Colombia, ambapo alisaini mkataba wa miaka minne na timu hiyo hadi mwaka 2028.

Blanco aliyefunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-25, alianzia soka katika akademia ya Club Deportivo Estudiantil kabla ya kujiunga na timu ya Ligi Kuu ya Aguilas Doradas, kisha baadaye akatolewa kwa mkopo kwenda Fortaleza FC.

Akiwa na Fortaleza FC, aliibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza Colombia (Categoria Primera B), baada ya kufunga mabao 13 kwa msimu wa 2022-23, kisha kuiwezesha timu hiyo kupanda daraja na kuchukua ubingwa kutokana na kiwango bora.

Kwa msimu wa 2022-23, Blanco alionyesha kiwango bora kilichovutia timu mbalimbali kuhitaji saini yake ambapo mbali na kuiwezesha Fortaleza kutwaa taji na kupanda daraja, alifunga jumla ya mabao 18, katika mechi 26, za mashindano yote.