Afisa Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Bw. Goodluck Assenga akitoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wakazi wa Manispaa ya Temeke walioshiriki katika Kongamano la Nishati Safi lililofanyika Agosti 30, 2025 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Kibasila, jijini Dar es Salaam. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)


Mgeni rasmi wa Kongamano la Nishati Safi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mtandao wa Uwezeshaji Wanawake Tanzania (TAWEN), Mhe. Janeth Mbene (kulia) akipewa elimu ya matumizi ya majiko yanayotumia nishati ndogo ya umeme.




Afisa Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Bw. Goodluck Assenga akitoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vikundi vya wajasiliamali wa Manispaa ya Temeke walioshiriki katika Kongamano la Nishati Safi lililofanyika Agosti 30, 2025 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Kibasila, jijini Dar es Salaam.

Maafisa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Temeke wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi wa Kongamano la Nishati Safi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mtandao wa Uwezeshaji Wanawake Tanzania (TAWEN), Mhe. Janeth Mbene (katikati).




………………
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke limeshiriki Kongamano la Nishati Safi kwa kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wafanyabiashara wadogo zaidi ya 70, wakiwemo Mama Ntilie, Baba Lishe, Wajasiriamali, pamoja na wanawake ambapo wamevutiwa na majiko hayo kutokana na ufanisi wake na matumizi ya nishati ndogo ya umeme.
Akizungumza Agosti 30, 2025, jijini Dar es Salaam, Mgeni rasmi wa Kongamano hilo, lililofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Kibasila, Manispaa ya Temeke, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mtandao wa Uwezeshaji Wanawake Tanzania (TAWEN), Mhe. Janeth Mbene, ameipongeza TANESCO Mkoa wa Temeke kwa kuongeza juhudi katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuleta tija.
Afisa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Bw. Goodluck Assenga, amesisitiza umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia kwani inatumia gharama nafuu tofauti na nishati nyingine ambazo si rafiki kwa mazingira.
“Majiko haya yana matumizi madogo ya umeme, pia bei yake ya kununua ni nafuu, hayaleti shoti ya umeme, hivyo ni rafiki kwa kila mtu na yanaweza kutumika hata maeneo ya vijini” amesema Bw. Assenga.
Nao wajasiriamali na wafanyabiashara katika kongamano hilo akiwemo Bi. Amina Juma wameipongeza TANESCO Mkoa wa Temeke kutoa elimu matumishi ya nishati safi ya kupikia, huku wakieleza kuwa mafunzo hayo yameongeza uelewa kuhusu matumizi salama ya majiko ya umeme ambayo yanatumia gharama nafuu.
Kupitia kongamano hilo, walipata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kutoka kwa maafisa wa TANESCO Mkoa wa Temeke kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo nishati safi ya kupikia.
TANESCO Mkoa wa Temeke imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuwahudumia watanzania kwa weledi na uwazi, huku ikisisitiza ushirikiano kati ya shirika hilo na wananchi kama nguzo muhimu ya kufanikisha upatikanaji wa huduma bora, salama na endelevu ya nishati ya umeme nchini.