…….
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepata tuzo kwa kuwa miongoni mwa Wizara zilizotoa washiriki wengi kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Menejiment ya Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA).
Wizara ya Ardhi ilitoa watumishi 56 kushiriki mkutano huo wa kitaaluma uliofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa Agosti 27, 2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa 13 wa mwaka chama cha TRAMPA.
Akipokea tuzo hiyo Ofisini kwake katika mji wa Serilali Mtumba jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema Wizara yake inaendelea kuwajali watumishi wa kada zote katika kushiriki mikutano mbalimbali ya kitaaluma ili kujifunza mambo mapya jambo alilolieleza litawasaidia watumishi kuboresha utendaji wao wa kazi.
“Tunaendelea kuwajali watumishi wa kada zote, mkitoka kwenda kwenye semina na mikutano ya taaluma zenu, mnapata fursa ya kujifunza” amesema Mhandisi Sanga
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka watumishi wa kada ya menejiment ya kumbukumbu na Nyaraka kutembelea masijala nyingine ili kuona jinsi wenzao wanavyofanya kazi ili kujifunza changamoto mpya.
Wakati wa kufungua mkutano wa 13 wa TRAMPA, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alitoa wito kwa watunza kumbukumbu wote nchini kuzingatia maadili ya kazi, kudumisha uadilifu na kulinda usiri wa taarifa zote zinazohifadhiwa kwani taarifa hizo ni nyenzo muhimu ya usalama wa Taifa na maendeleo ya nchi.
Alieleza kuwa, Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) kinabeba dhamana kubwa ya kuhakikisha nyaraka na kumbukumbu zote muhimu za Serikali pamoja na taasisi binafsi zinatunzwa kitaalamu na zinahifadhiwa.