ZOTE NDANI KUWAPA BURUDANI KEDEKEDE VIJANA

Kampuni ya Startimes imezindua kampeni mpya iitwayo Zote Ndani, ikiwapa watazamaji ofa maalum kupitia vipindi mbalimbali vya burudani, michezo, tamthilia na vipindi vya watoto.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Meneja Masoko wa Startimes, David Malisa, alisema kampeni hiyo inaleta vipindi vya kipekee sambamba na michezo ya kimataifa itakayorushwa kupitia kisimbuzi cha Startimes.

“Tumejipanga kuonesha mechi kali kutoka Ligi Kuu ya England, La Liga na Bundesliga kupitia kisimbuzi chetu cha familia,” amesema Malisa.

Mbali na michezo, Startimes pia imetambulisha tamthilia mbili kubwa kutoka Uturuki ambazo zimetafsiriwa kwa Kiswahili, ikiwemo Shadel T na Sagado Hadel Queen.

Kwa upande wake, Godfrey Lugalabamu maarufu kama ‘Mc Gara B’, amesema msimu mpya wa Hello Mr. Right utarejea na maudhui mapya yenye msisimko.

“Nimekuwa sehemu ya Hello Mr. Right tangu msimu wa kwanza. Baada ya kupumzika msimu wa sita, mashabiki walitaka nirejee—na sasa natangaza rasmi kwamba nimerudi kwa ajili ya kuzalisha mahusiano mapya. Msimu huu wa saba utakuwa na mambo mengi ya kushangaza,” amesema Mc Gara B.

Naye, Maimartha Jesse, mmoja wa watangazaji wa kipindi hicho, alisisitiza umuhimu wa washiriki kuwa wazi kwa familia zao kabla ya kushiriki.

“Washiriki wanapokuja Hello Mr. Right tunawahimiza wazungumze na wazazi wao mapema, kwani nia ya shindano hili ni kuona watu wakikutana, kupendana na hatimaye kufunga ndoa. Pia tunahakikisha wanapima afya kabla ya kuingia kwenye mahusiano ya ndoa,” amesema Maimartha.

Kwa upande wa vipindi vya watoto, Startimes imetangaza kuonesha katuni mpya kupitia ist Kids, ikiwemo Mbabe, sambamba na ofa mbalimbali na punguzo la bei kwa kisimbuzi cha familia.