Akutwa ameuawa, mwili kutelekezwa relini Kigoma

Kigoma. Mtu mmoja mwanamume amekutwa ameuawa kwa kukatwakatwa kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiojulikana, kisha mwili wake kutelekezwa katika Mtaa wa Butunga relini, Kata ya Kibirizi.

Agosti 31, 2025, mwili wa mtu huyo aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 45 mpaka 50 ulikutwa katika mtaa huo na watu waliokuwa wakipita kuelekea katika shughuli zao, huku akitajwa kuwa alikuwa fundi seremala Mtaa wa Gezaulole, Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, SACP Filemon Makungu, amesema tayari ndugu wa marehemu wamekabidhiwa mwili, huku akisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kuwabaini wahusika wa tukio hilo.

‘’Ameshatambulika na ndugu zake baada ya uchunguzi wa kitabibu kukamilika. Sababu ya kifo chake bado haijafahamika kwa sababu amekutwa relini hapo. Hatujathibitisha lakini bado upelelezi unaendelea, ukikamilika ndio utatwambia alitokea wapi, alianza wapi, akaenda wapi,’’ amesema SACP Makungu.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Butunga, Hamis Yasin, ametoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka waliohusika na tukio hilo.

Aidha, ametoa wito pia kwa Jeshi la Polisi kusambaratisha makundi ya vijana wanaojihusisha na uvutaji wa bangi na uchezaji kamari kwa kuwa makundi hayo yamekuwa yakihusishwa na matukio ya kihalifu.

‘’Mtu huyo anakadiriwa kuwa ma umri kati ya miaka 45 mpaka 50, sikumfahamu kwa sura na sijajua sababu ya kuuawa kwake, japo mwili umekatwakatwa sana, miguu yake.

 ‘’Eneo hilo la relini limekuwa na matukio mengi na hasa yakitokea Mtaa jirani wa Gungu, na ninashauri viongozi wenzangu wa Serikali ya Mtaa tushirikiane kwa pamoja kufanya doria mchana na usiku ili kupunguza matukio ya ukabaji na mauaji,’’ amesema Yasin.