Dar es Salaam. Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU), na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), imezindua awamu ya pili ya Mradi wa Stosar (Stosar II) wenye lengo la kuhakikisha biashara salama na endelevu ya mazao ya kilimo na vyakula.
Uzinduzi huo umefanyika Septemba 2, 2025 jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Edwin Mhede.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dk Mhede amesema mradi huo utashughulikia maeneo muhimu ikiwemo afya ya wanyama, afya ya mimea, lishe, pamoja na kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Pia utahusisha uchunguzi na ufuatiliaji wa magonjwa, udhibiti wa ubora na upatikanaji wa masoko ya kikanda na kimataifa.
“Mradi huu unalenga kujenga mifumo imara ya usafi na usalama wa chakula, si tu kwa mazao ya kawaida, bali pia mifugo na samaki. Hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha walaji wanapata vyakula salama na vinavyokidhi viwango vya kimataifa,” alisema Dk. Mhede.
Akitathmini utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo iliyozinduliwa mwaka 2018, Dk. Mhede alisema zaidi ya wataalamu 150 nchini wamenufaika kupitia mafunzo mbalimbali, ingawa utekelezaji wake ulipata changamoto kutokana na mlipuko wa Uviko-19.
Alibainisha kuwa awamu ya pili inalenga kujenga mfumo wa kisasa utakaowezesha taarifa za usalama na ubora wa chakula kupatikana kwa wakati, na kusaidia wadau kufanya maamuzi sahihi yanayotokana na ushahidi wa kisayansi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Asilia katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Lamine Diallo, amesema EU itaendelea kushirikiana na Tanzania na nchi nyingine za SADC katika kuendeleza kilimo.
“Awamu hii mpya inajengwa juu ya mafanikio ya Stosar I uliokamilika mwaka 2024. Kupitia Stosar II, tunataka kuona matokeo ya moja kwa moja na utekelezaji wa sera ya kikanda ya kilimo ya SADC, ambayo itawanufaisha wananchi wa Afrika Mashariki na Kusini,” alisema Diallo.
Naye Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania, Dk Nyabenyi Tito Tipo, alisema mradi huo umesaidia kuimarisha mifumo ya SPS licha ya changamoto kadhaa zinazoweza kuchelewesha upatikanaji wa masoko ya kimataifa.
“Kwa miaka mitano iliyopita, wakulima zaidi ya 200 wa parachichi wameuza mazao nje ya nchi, hususan Afrika Kusini na India. Pia tumeimarisha mifumo ya afya ya mimea na mifugo kwa kuhakikisha hakuna milipuko ya mafua hatari ya ndege wala ugonjwa wa Fusarium wilt kwa ndizi. Kampeni ya chanjo ya Peste des Petits Ruminants (PPR) pia imeongeza uthabiti wa mifumo ya afya ya wanyama,” amesema Dk Tipo.
Ameongeza kuwa hatua hizo zimeweka msingi thabiti kwa Tanzania kuingia kwenye masoko mapya ya kimataifa, yakiwemo ya Mauritius, hatua itakayowezesha kuongeza pato la wakulima na kuchochea uchumi wa taifa.