CCM Kinondoni kuanza na makundi kisha kampeni

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, kimesogeza mbele ratiba ya kuanza kampeni zake kikisema kinatoa nafasi ya kuvunja makundi yaliyoibuka kipindi cha kura za maoni.

Kampeni rasmi katika majimbo ya Kawe na Kinondoni zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi Septemba 13 na 14, 2025, kama sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Septemba 2, 2025, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Shaweji Mkumbara amesema  chama kimeamua kuanza upya kwa kuondoa makundi yote yaliyosababishwa na kura za maoni ili kuhakikisha mshikamano wa wanachama.

“Kwa sababu kulikuwa na makundi kipindi cha kura za maoni, sasa tumeamua kuvunja kila kitu. Chama kinapita kata kwa kata kuhakikisha mshikamano wa wanachama wetu. Tunataka kuingia kwenye uchaguzi tukiwa kitu kimoja,” amesema Mkumbara.

Ameongeza kuwa kampeni hizo zimepangwa kwa makusudi ya kujenga mshikamano, kuongeza morali ya wanachama na kuimarisha nafasi ya chama kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Agosti 31, 2025, CCM Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Abbas Mtevu, kilizindua kampeni katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sokoine, Temeke, tukio lililohudhuriwa na wabunge pamoja na madiwani wa mkoa huo. Hii ilikuwa ni mwendelezo wa uzinduzi wa awali uliofanyika Agosti 28, 2025 katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, uliotambulisha rasmi kampeni za chama hicho ngazi za chini mpaka Taifa.

Katika hatua hiyo, CCM ilieleza lengo lake la kuhakikisha wagombea wake wote kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais wanapata ushindi na kuendelea kuongoza Serikali.

Baadhi ya wanachama wa chama hicho katika Kata ya Mzimuni, Kinondoni wameeleza kuridhishwa na mwelekeo huo.

“Mara nyingi makundi yamekuwa chanzo cha mpasuko ndani ya chama. Safari hii tumeona viongozi wetu wamejipanga, ndiyo maana wameamua kuchelewesha kampeni ili kwanza kurekebisha tofauti zetu na kutuunganisha pamoja. Jambo hili linatupa matumaini makubwa ya ushindi,” amesema Zainabu Kisoki.

Kwa upande wake, Hamis Salum kutoka Kinondoni alisema mkakati unaoendelea umeongeza nguvu kwa wanachama wa kawaida kushiriki kikamilifu.

“Kinachopigiwa kelele sasa ni mshikamano. Hata waliokuwa wamekaa pembeni baada ya kura za maoni wanatakiwa kurudi tuwe kitu kimoja. Tukianza kampeni tutapita kila kichochoro, hatuachi kitu hadi siku ya mwisho,” amesema.