Chaumma yakumbushia uhaba wa sukari ikitoa njia kukomesha ikishika dola

Morogoro. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimewakumbusha wananchi madhila waliyopitia kuzuiwa sukari hadi zaidi ya Sh6,000 kwa kilogramu moja, kikisema endapo itaunda Serikali mabonde yaliyopo Mkoa wa Morogoro yatawekewa mkakati bora wa kilimo cha miwa.

Kauli hiyo ya Chaumma imetolewa na mgombea mwenza wa kiti cha urais Devotha Minja leo Septemba 2, 2025 akiwa wilaya ya Kilosa kwenye kampeni za kunadi sera za chama chake, ili Watanzania kukichagua chama hicho kiunde Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu

Sakata la sukari alilokumbushia mgombea huyo kama kete ya kuwashawishi wananchi kukiamini chama chake, lilitolekea mwanzoni mwa mwaka jana ambapo licha bei kuwa juu bidhaa hiyo wananchi walilazimika kupanga foleni kupata huduma baadhi ya maeneo.

Hata hivyo, Serikali katika kukabiliana na adha hiyo kwa wananchi, ilitoa vibali maalumu kwa wafanyabiashara kuingiza sukari nchini na kuuzwa kwa bei elekezi.

Wakati hali hiyo ikiwa imesahaulika mgombea huyo ameikumhusha akishangaa sukari kuuzwa zaidi ya Sh7,000 akihoji sababu ya sukari mkoa wa Morogoro kuwa juu na kuna viwanda vya sukari.

“Morogoro mnaviwanda Mtibwa na Kilombero lakini bei ya sukari ni kubwa Ruaha (Morogoro) kuliko Dar es Salaam ni maajabu,pamoja na kwamba tuna viwanda kuna wakati sukari iliuzwa hadi Sh7,000 maeneo mengine hadi Sh10,000,

“Sukari iuzwe hadi Sh10,000 wakati tuna viwanda inawezekana tumekuwa na shida kwenye sukari, kuna wakati hatuna misimu ya sukari, badala  Chama cha Mapinduzi (CCM) kiweke utaratibu mzuri wa kupata sukari wafanyabiashara wanakuwa watu walanguzi,” amesema.

Mgombea huyo amesema ili kukomesha changamoto hiyo Serikali ilipaswa kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na uhakika wa bidhaa hiyo kwa wananchi.

Ameongeza kuwa Chaumma itakapopewa ridhaa na wananchi kuunda Serikali,wakulima watawezesha kulima miwa kwa wingi na mabonde yote mkoani hapo yanatumika kwa kilimo cha miwa.

Kwa upande wake Mgombea Ubunge Jimbo la Mikumi kupitia Chaumma Abbas Nyamoga ameowaomba wananchi wa Jimbo hilo kukiamini chama chake ili wakatatue kero zinazowasibu.

Kero kubwa aliyoitaja ni vijana kukosa ajira na kukimbilia michezo ya kubahatisha Hali aliyoielezea kuwa haipaswi kuwa hivyo kwani vipo viwanda vingi mkoani hapo lakini wanaonufaika ni wageni kitendo alochotafsiri kuwa sio sahihi.