DAWASA yadhibiti mivujo ya maji Bagamoyo

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Chalinze imedhibiti mivujo ya maji katika maeo ya Kiwangwa, Mwavi na Mwetemo wilayani Bagamoyo.

Akizungumzia kazi hiyo, Kaimu Meneja wa Mkoa wa Kihuduma Chalinze, Mhandisi Hafidhi Mketo amesema udhibiti huo umefanyika katika mabomba ya nchi 3′, 2′ na moja 1 na nusu ambayo wasambaza maji moja kwa moja hadi kwa wateja wa maeneo hayo.

“Kazi hii ina lengo la kusaidia kuongeza upatikanaji wa maji kwa wateja kwa kudhibiti upotevu wa maji, lakini pia tumeendelea kutoa elimu kwa wananchi ya ulinzi wa miundombinu ya maji pamoja njia rasmi za kutoa taarifa wakiona uharibifu wa miundombinu ili tuokoe maji yasipotee,” amesema Mhandisi Mketo.

Kwa niaba ya wenyeviti wa maeneo hayo, Mwenyekiti wa kijiji Kiwangwa, Ndugu Ayubu Mziwanda amepongeza kasi ya Mamlaka katika kuimarisha huduma kwa kukarabati miundombinu kwa wakati na kupunguza upotevu wa maji katika maeneo yao ambapo kwa sasa huduma imeendelea kuimarika kwa wananchi.

Mpango mkakati wa Mamlaka ni kupunguza upotevu wa maji yanayozalishwa kutoka asilimia 52 ya sasa hadi kufikia asilimia 35 katika mwaka huu wa fedha 2025/2026 ili kuimarisha utoaji wa huduma ya uhakika kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.