UONGOZI wa Mbeya City upo katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa Deusdedity Okoyo aliyekuwa akiichezea KMC msimu uliopita ili kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo cha kati.
Kama uhamisho wa Okoyo utakamilika atakutana na ushindani wa wachezaji wengine wanaotajwa kujiunga na kikosi hicho Omary Chibada anayedaiwa kutokea Kagera Sugar, Jeremie Ntambwe Nkolomoni ambaye ni raia wa DR Congo aliyekuwa Coastal Union na Minigeria Paschal Onyedika.
Chanzo ndani ya Mbeya City kimesema tayari wamesajili wachezaji wa viwango ili kurejea kwa kishindo katika Ligi Kuu na kuonyesha ushindani dhidi ya timu pinzani.
“Mazungumzo baina yetu na Okoyo yanakwenda vizuri. Ni vitu vidogo ndivyo vimesalia ili kulikamilisha jambo hili. Ni mchezaji aliye na kipaji kikubwa na ujuzi tunaamini anaweza kuwa msaada mkubwa katika kikosi chetu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Mbali na Okoyo kikosi hicho kina wachezaji wengi wazoefu akiwamo Beno Kakolanya na Yahya Mbegu waliokuwa Singida Black Stars pamoja na Eliud Ambokile alikuwa na timu Ligi ya Championship. Naamini tuna kikosi cha kuonyesha ushindani na kutupatia ushindi.”
Timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita wa Ligi ya Championship, ambapo ilipanda pamoja na Mtibwa Sugar kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kusota nje ya mashindano hayo kwa msimu wa 2022-23.