Dk Mwinyi aahidi akiondoka madarakani hataacha madeni serikalini

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ametaja kinachompa ujasiri wa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ni kutokana na kufungua akaunti maalumu ya kulipa madeni, akisisitiza kuwa iwapo akiondoka madarakani hataacha deni lolote la Serikali.

Dk Mwinyi amesema baada ya kuona kuna haja ya kutekeleza miradi kupitia utaratibu wa mikopo, alifungua akaunti maalumu ambayo kila mwezi walikuwa wakiweka Dola milioni 10 za Marekani, lakini baada ya kuona miradi inayotekelezwa imekuwa mikubwa, akaagiza na kwa sasa wanaweka Dola milioni 15.

Dk Mwinyi amesema hayo leo, Septemba 2, 2025, Ikulu ya Zanzibar, alipozungumza na wahariri na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Zanzibar na Tanzania Bara.

“Dhamira yangu, nitaondoka katika uongozi, siachi deni hata senti tano. Mwanzoni tulifungua akaunti, kila mwezi tunaweka Dola za Marekani milioni 10, lakini baadaye tukaona hazitoshi, tukaongeza mpaka dola milioni 15,” amesema.

Dk Mwinyi amesema kwa mwaka akaunti hiyo inakuwa na zaidi ya Dola milioni 180.

“Sasa una kiasi hicho cha fedha, unashindwa nini kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo?” amehoji.

Amesema wakati anaingia madarakani mwaka 2020, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), wakati huo ikiitwa Bodi ya Mapato (ZRB), ilikuwa ikikusanya Sh20 bilioni kwa mwezi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikuwa ikikusanya Sh25 bilioni.

Amesema sasa ZRA inakusanya Sh80 bilioni, huku TRA ikikusanya zaidi ya Sh50 bilioni kwa mwezi.

Kutokana na uwezo walionao wa kulipa madeni, amesema takribani benki zote zimekuwa zikijitokeza zikihitaji kuikopesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) baada ya kuona uwezo wake wa kulipa.

Ametoa mfano wa baadhi ya miradi inayotekelezwa na kutumia fedha nyingi kuwa ni ujenzi wa Bandari ya Mangapwani, ambao thamani yake ni Dola milioni 300, miradi ya maji inayotekelezwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa na thamani ya Dola milioni 27, na mwingine unatarajiwa kutekelezwa mkoani Kusini Unguja ukiwa na thamani ya Dola milioni 55.

Rais Mwinyi amesema siri ya mafanikio na uwezo wa kutekeleza miradi hiyo ni kukusanya vyema mapato, kuyasimamia na kuyatumia vyema bila kufanya ubadhirifu.

Amesema: “Ukikusanya vizuri unaweza kukopesheka, na ukikopa una uwezo wa kufanya miradi yenye tija.”

Nyingine amesema walihakikisha nchi inakuwa na amani, mshikamano na umoja miongoni mwa Wazanzibari, kwani hata maeneo yaliyokuwa yana mifarakano yametulia.

“Siri ya kwanza ni amani, umoja na mshikamano. Huwezi kufanya maendeleo yoyote ikiwa hakuna amani ndani ya nchi. Hata maeneo ambayo yalikuwa yana mifarakano, lakini sasa yametulia na kuna mshikamano,” amesema.

Amesema nia yake ni kuifanya Zanzibar mambo yote yaende kidijitali, hivyo mambo yote yanayofanywa yanaelekea huko katika sekta zote.

Ametaja sekta ambazo zimeanza ni ya elimu, ambayo kuna shule zinajengwa na kufundisha kwa teknolojia, hivyo kusaidia kukabiliana na upungufu wa walimu.

Amesema wamejenga shule ya Mtakuja, ambako teknolojia hiyo inatumika, na wapo katika ujenzi wa nyingine 20 kwa majaribio, mpango ukiwa kujenga shule zote katika mfumo huo.

Amesema sekta zote za uchumi wa buluu, zikiwamo utalii, uvuvi, usafirishaji na bahari, wanahakikisha zinakua na kufikia viwango vya juu.

Katika sekta ya maji, amesema licha ya kuwa kuna baadhi ya maeneo hayajakaa sawa, lakini wanajivunia hali ilivyo sasa tofauti na ilivyokuwa kipindi wanaingia madarakani.

Kuhusu ufaulu katika elimu, amesema hali ilivyo ni tofauti na ilivyokuwa, akieleza kuwa matokeo yaliyokuwa yakitangazwa, shule 10 za mwisho, nane zilikuwa zinatoka Zanzibar, lakini sasa hakuna jambo kama hilo na ufaulu umefikia asilimia 98 katika mtihani wa kidato cha sita.

Amesema bado kuna changamoto ya wataalamu ndani ya nchi, lakini mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kila sekta inapata wataalamu na wameanza kuwaandaa kwa kujenga shule za amali kila wilaya, ambazo vijana wengi wanapata ujuzi.

Amesema vijana hao ndio watakaotumika kwenye miradi inayojengwa na inayotarajiwa kujengwa katika sekta tofauti.

Kuhusu madai ya miradi kufanyika bila kutangazwa zabuni, Dk Mwinyi amesema hakuna iliyotekelezwa kwa kukiuka sheria, isipokuwa ni suala la uelewa.

Amesema kuna aina tatu za zabuni, akizitaja kuwa ni ya wazi, inayotangazwa waziwazi na kampuni zinaomba na kushindanishwa. Pia, zabuni maalumu ambayo mhusika anaweza kuchagua kampuni tatu zenye uwezo, kisha akazishindanisha na kupata moja, na nyingine ni ya kuchagua kampuni moja yenye uwezo, kisha inapewa kazi.

“Kwa hiyo hili ni suala la uelewa, hakuna zabuni imekiuka sheria. Zabuni zote hizi zipo kwenye sheria ya ununuzi, na ipo baadhi ya miradi inalazimika tuchague, kwani hata ukitangaza hakuna kampuni za hapa nchini zenye uwezo wa kufanya kazi,” amesema.

Dk Mwinyi amesema suala la wataalamu kujitosheleza bado, ndiyo maana wameamua kutumia kampuni binafsi kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma, akitoa mfano katika sekta ya afya ambayo yameonekana mafanikio makubwa.

Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, amesema kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuhubiri amani, mshikamano na umoja ili wavuke salama.

“Viongozi wa dini, wanasiasa na waandishi wa habari, kila mmoja ahubiri amani, kuwasihi wananchi kufanya uchaguzi wa amani. Tukifanya hivyo tutavuka salama,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema wamefanya ziara katika miradi, wamejionea kwa macho kilichofanywa katika utawala wa awamu ya nane.

Balile amesema wamepitia ilani ya CCM ya mwaka 2020/25, wamebaini yapo mambo mengi yamefanyika na kupitiliza ikilinganishwa na ahadi zilizotolewa, akitoa mfano wa ujenzi wa barabara zaidi ya kilometa 1,000, ilhali ilani ilisema kilometa 99.