Dk Nchimbi aeleza sababu Samia kuwa chaguo sahihi

Itilima. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema kazi kubwa aliyoifanya Mwenyekiti wa chama hicho na Rais Samia Suluhu Hassan inawapa ahueni ya kuomba kura.

Aidha Dk Nchimbi amesema Rais Samia ameboresha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa mbalimbali hali inayochagiza kuvutia zaidi uwelezaji. Ameikamilisha miradi ya kimkakati iliyoachwa na mtangulizi wake.

Samia ambaye alikuwa Makamu wa Rais, Machi 19, 2021 aliapishwa kuwa Rais kuchukua nafasi ya Rais John Magufuli, aliyefariki dunia siku mbili nyuma yaani Machi 17, katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyoma, jijini Dar es Salaam.

Magufuli alifariki dunia baada ya kuumwa gafla tatizo na moyo. Mwili mwili wake, ulizikwa nyumbani kwao,  Chato, mkoani Geita.
Wakati Magufuli anafariki dunia, aliacha miradi mbalimbali ikiwemo Bwawa la Nyerere, Daraja la Tanzanite (Dar es Salaam) na Daraja la Magufuli (Mwanza).

Dk Nchimbi amemwelezea Rais Samia leo Jumanne, Septemba 2, 2025 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyikia Stendi ya mabasi ya Lagangabilili, Jimbo la Itilima, Mkoa wa Simiyu.

“Amekiongoza chama kukidhi mafanikio ya Watanzania. Mwenyekiti angefanya chini ya kiwango, Rais angefanya chini ya kiwango leo tusingekuja hapa tena kuomba kumchagua,” amesema Dk Nchimbi.

Katibu Mkuu huyo wa zamani wa CCM amesema chini ya Rais Samia 

Itilima imepata hospitali, vituo vya afya, ujenzi wa barabara, madarasa jambo linalowafanya watembee kifua mbele kurudi kwa Watanzania kuomba tena ridhaa.

Amegusia ushirikiano wa Tanzania nje akisema:”Tuna mahusiano mazuri na majirani zetu wa Afrika Mashariki, Jumuiya za Kikanda, tuna mahusiano mazuri na mataifa mbalimbali. Kwa kweli hatumdai, amefanya kazi kubwa ndani na nje.”

Huku hotuba yake ikikatishwa kutokana na ushangiliaji, Dk Nchimbi akasema:”Amefanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya kimkakati, Bwawa la Nyerere alilopokea likiwa kama asilimia 33 lakini sasa kazi imekamilika. Wenzetu wa Mwanza lile Daraja la Magufuli limekamilika.”

“Huduma za afya mama na mtoto zimeboreshwa. Hospitali za Kanda na za mikoa zimeboreshwa sana na huduma za kibingwa zinatolewa na kidogo sana ndio wanakwenda labda Dar es Salaam,” amesema.

Katika kuhitimisha Dk Nchimbi ambaye amewahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali akasema:” (Rais Samia) amemaliza mitano, tumpe mitano tena atupeleke mbali zaidi.”

Mgombea ubunge wa Itilima, Njalu Silanga amesema kuna miradi mikubwa imefanyika Itilima ambayo kila mmoja anaiona.
“Tulikuwa na ttizo kubwa la madaraka, pamoja na huduma nzuri hospitalini walikuwa wanakwama kuzifikia lakini madaraja kwa sasa yamefika 52 kutoka 12. Barabara zilikuwa kilomita 500 lakini sasa zimefika 857,” amesema Silanga.

“Madiwani 19 kati ya 22 wamepita bila kupingwa na mimi mwenyewe na hii inatokana na kazi kubwa aliyofanya Rais Samia. Licha ya jimbo hili kuwa na historia ya upinzani lakini kwa kazi kubwa basi wakasema watapita bila kupingwa,” amesema Silanga.

Madiwani hao 19 na mbunge wanasubiri kupigiwa kura ya ndio au hapana, Jumatano ya Oktoba 29, 2025 siku ya upigaji kira.
“Lakini niwaambie licha ya kupita bila kupingwa, tunakwenda kufanya kampeni kubwa sana ili kuhakikisha Rais Samia anapata kura nyingi na za kishindo,” amesema Silanga huku akishangiliwa na mamia ya wanachama na wananchi.

Awali, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed akimkaribisha Dk Nchimbi kuzungumza amesema Itilima yamefanyika mengi ikiwemo kwenye barabara, maji, huduma za afya:”Na Oktoba tunakwenda kutiki tu kwa sababu Rais Samia amefanya mambo makubwa ambayo kila mmoja anayaona maendeleo.”

Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema Rais Samia anapambana kumtua ndoo mama kichwabi, anajenga madaraja ili Watanzania wasafiri, anahangaika huku na huko kutafuta fedha za kutatua matatizo yetu.

“Utulivu na amani iko chini ya Rais Samia, utulivu huu ambao Baba wa Taifa alituachia, niwaambie wana Itilima utakuwa salama chini ya Rais Samia,” amesema Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema.