Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa amesema kampeni za uchaguzi wa mwaka huu, zimekosa chama kinachozungumza masuala muhimu kwa raia.
Dk Slaa anasema hayo, wakati chama chake kikiwa si miongoni mwa vinavyoshiriki uchaguzi kutokana na ajenda yake ya kudai mabadiliko mifumo ya uchaguzi maarufu kama ‘No reforms no election.’
Chini ya ajenda yake hiyo, chama hicho kiliweka sharti la kurekebisha kwanza kasoro za kisheria na kikatiba kabla ya uchaguzi na hivyo hakikusaini kanuni za maadili na kutupwa nje ya mchakato.
Mwanasiasa huyo ameyasema hayo leo, Jumanne Septemba 2, 2025 alipozungumza katika Baraza la Kidigitali lililohusisha kanda 10 za chama hicho, lililofanyika kwa njia ya mtandao.
Amesema kwenye kampeni zinazoendelea, vyama vya siasa havitamki masuala muhimu hasa haki za raia, huku vingine vikiyataja juujuu badala ya kuzama kwa kina.
“CCM yenyewe imekuja na ilani yake inaorodhesha tutafanya moja, mbili, tatu, nne, tano, sita… lakini watafanyaje, wananchi wameshirikishwaje, yote hayo hayaelezwi,” amesema.
Amesema katika kampeni hizo, hayasikiki masuala muhimu yanayowasumbua Watanzania, kwani majukwaa hayo yanapaswa kuwa matibabu ya matatizo.
“Matatizo makubwa nchini mwetu ni rushwa, uuzwaji wa rasilimali zetu na ardhi, yote hayo huwezi kuyasikia kwenye kampeni. Lakini hata yale yanayotajwa yanachekesha,” amesema.
Wakati Dk Slaa akisema hayo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wakizungumza na gazeti la The Citizen wamesema baadhi ya ahadi zinaonekana kutokulingana na hali halisi ya kiuchumi ya nchi.
Mathalan, Mgombea mwenza wa Chaumma, Devotha Minja, ameahidi kushusha bei ya mchele hadi kufikia Sh500 kwa kilo, wakati hali ya soko inaonyesha bei ya jumla ni takribani Sh2, 200 na rejareja inafikia mpaka Sh3, 000.
“Haiwezekani kushusha bei kwa zaidi ya mara sita bila kuathiri maisha ya wakulima,” amesema mtafiti wa kilimo David Mallya huku akiwashauri wapiga kura kuwa makini na ahadi zisizo na maelezo ya jinsi ya kuzitekeleza.
Wachambuzi wanasema kampeni zimekuwa kama jukwaa la maigizo, ambalo ahadi za ajabu ndizo zinazovutia vyombo vya habari.
“Katika demokrasia changa, maneno ya kutia chumvi hupata nafasi. Wagombea wanajua maneno ya kishindo yatavutia mitandaoni, hata kama hayatekelezeki,” amesema mchambuzi wa utawala, Rose Mwansasu.
Ameongeza: “Lakini wananchi lazima watofautishe kati ya burudani na sera.”
Mchambuzi mwingine, Dk Amina Kuzweka amesema: “Ahadi hizi ni kubwa mno, lakini swali ni kama zinawezekana kiuchumi na kiutawala katika mazingira ya Tanzania ya sasa.”
Kwa mfano, kugawa ardhi kwa kila kijana kunahitaji mipango mikubwa, upimaji wa viwanja na rasilimali ambazo Serikali bado haijafikia lengo mpaka sasa.
Visiwani Zanzibar, mgombea urais kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Said Soud Said ameibua mjadala baada ya kuahidi kuruhusu kilimo cha bangi kwa matumizi ya kiuchumi, akidai hatua hiyo itaokoa maisha na kuongeza mapato ya Serikali.
Hata hivyo, chini ya sheria za Tanzania, bangi bado haramu na imetajwa kama dawa ya kulevya. Hivyo wanasheria wanapinga ahadi hizo wakiziona kama ndoto za mchana.
“Hii si tu kwamba haiwezekani kisheria, bali pia inapingana na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia,” amesema Wakili Hassan Mzee.
Kauli nyingine ni kuhusu kupiga marufuku vitanda vya sita kwa sita Zanzibar, hoja iliyozua kicheko na maswali. Mgombea huyo amedai vitanda hivyo vimechangia kupungua kwa viwango vya uzazi visiwani humo.
“Wakati nitakapokuwa Rais, nchi hii haitakuwa na vitanda vya sita kwa sita; vitanda havitazidi futi nne. Zamani mababu zetu walitumia vitanda vya futi mbili na nusu au tatu. Leo Zanzibar hatuzaliani kwa sababu ya vitanda hivi vikubwa, maana yake nini?” alihoji.
Katika kampeni hizo, mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kununua matrekta milioni 10 ndani ya miaka mitano, ili kuboresha kilimo na kupunguza gharama kubwa za kukodisha vifaa.
“Lengo ni kuwaondolea mzigo wakulima ambao hukodisha kwa gharama kubwa, hadi Sh80, 000 kwa ekari, gharama ambazo tayari zimeanza kushuka na sasa imefikia Sh40, 000, baada ya Serikali kuanza kuweka vituo vyake vya matrekta” alisema Samia akiwa kwenye kampeni wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma, ahadi inayotofautiana na za vichekesho.
Katika hatua nyingine, Dk Slaa amesema Chadema haikuingia kwenye uchaguzi na sio bahati mbaya, bali imeamua na hilo linathibitisha kuwa chama hicho hakina uchu wa madaraka.
“Tanzania ina mahitaji makubwa ya kuongozwa, nashukuru angalau wana Chadema hawana uchu wa madaraka na wamejitoa sadaka, kwa hiyo ubunge na udiwani si kipaumbele kwao,” amesema.
Amesema uamuzi wa chama hicho kuzuia uchaguzi iwapo mabadiliko hayatafanyika ni mtakatifu kwa kuwa unalenga kuunufaisha umma.
“Vyama visivyojali nguvu na mamlaka ya umma, tuviache tu vipokee vinayoyataka wala tusikatishwe tamaa, sisi tunajua tunalenga nini,” amesema Dk Slaa.
Chadema kuwaenzi mashujaa
Hatika hatua nyingine, Chadema kimeanza kampeni ya kuvaa nguo nyekundu kwa siku saba kuanzia kesho Septemba 3, ikiwa ni ishara ya kuwaenzi mashujaa wake.
Hatua ya kuvaa rangi hiyo, imeelezwa na Mkurugenzi wa Habari, Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia kuwa ni kutekeleza maazimio ya kamati kuu ya chama hicho iliyoelekeza kuifanya Septemba 7, siku ya kusherehekea mashujaa waliopigania haki na demokrasia katika uongozi wao.
Kuelekea sherehe hiyo, amesema watahamasisha wanachama na wananchi kuvalia nguo nyekundu kuanzia Septemba 3 hadi 7, mwaka huu.
“Tutazungumzia mageuzi na kwa nini Chadema hatujaingia kwenye uchaguzi wa mwaka huu,” amesema.
Akisisitiza hilo, Dk Slaa amesema nguo hizo zivaliwe pia kama ishara ya utetezi wa watu waliopoteza maisha kwa dhuluma.
Wakati mashujaa hao wakikumbukwa, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje amesema yeyote aliyepo ndani ya Chadema hadi sasa anastahili kuitwa shujaa.
“Mtu yeyote aliyepo ndani ya chama chetu hadi leo ni shujaa. Kwa hiyo tunao mashujaa ambao bado wapo na wale wengine waliofariki au kupata ulemavu,” amesema.
Pamoja na magumu yanayoiabili nchi, amesema angalau kuna faraja kutoka kwa viongozi wa dini wanaotoka hadharani kupinga yanayotokea nchini.
Katika mazingira hayo, amesema ni muhimu wanachama wa chama hicho kutiana moyo kwa kuwa kuna maumivu makali ya kuendelea kuwa mpinzani.
“Kila familia kuna kovu na mengine yanaonekana na mengine hayaonekani, lakini kote kuna matatizo. Tunapokutana kwenye mihadhara tuwatie moyo wana-Chadema,” amesema.
Akizungumzia hilo, Wenje amesema hawapaswi kukata tamaa kwa sababu kufanya hivyo ni kuwasaliti watu mbalimbali waliowahi kupoteza maisha.
“Hali ni ngumu na inawezekana huko tunakoenda hali inaweza kuwa ngumu zaidi, lakini panapo giza zaidi ujue mwanga unakaribia,” amesema.