
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika uongozi wa Awamu ya Nane yametokana na kudumu kwa amani, mshikamano na utulivu nchini.
Akizungumza leo, Septemba 2, 2025, Ikulu Zanzibar alipokutana na jopo la wahariri na waandishi wa habari, Dkt. Mwinyi alisema hali hiyo imeiwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa. Aidha, alieleza kuwa ukusanyaji bora wa mapato na matumizi sahihi ya fedha za Serikali umeimarisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Dkt. Mwinyi alisema kwa muda mrefu Zanzibar ilikabiliwa na changamoto za maendeleo kutokana na wananchi kutoonesha mshikamano pamoja na ukosefu wa utulivu. Hata hivyo, alisema kwa sasa Serikali ina uwezo mzuri wa kukopa na kuendesha miradi mikubwa kutokana na ukusanyaji thabiti wa kodi. Hatua hiyo imeijengea Zanzibar heshima ya kuaminika kimataifa kwa kulipa madeni kwa utaratibu bora, ambapo Serikali huweka akiba ya dola milioni 15 kila mwezi kwa ajili ya akaunti ya usimamizi wa madeni.
Akizungumzia mipango ya awamu ijayo endapo atapata ridhaa ya wananchi, Dkt. Mwinyi alisema Serikali itazingatia kumaliza changamoto katika sekta muhimu ikiwemo maji, afya, elimu na miundombinu ya barabara. Pia alieleza kuwa Serikali imekusudia kuongeza nguvu katika kuendeleza wataalamu wa ndani na kuimarisha vyuo vya amali ili vijana wapate elimu ya kiufundi na stadi za kazi zitakazowawezesha kujiajiri na kuajirika.
Kuhusu uchaguzi mkuu ujao, Rais Dkt. Mwinyi alitoa wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa na waandishi wa habari kuendelea kuhubiri amani na mshikamano kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Mkutano huo ulihusisha wahariri na waandishi kutoka vyombo mbalimbali, baada ya jopo hilo kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali Unguja na Pemba.