Dodoma. Kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Jiji la Dodoma imehamia kwenye masoko na vituo vya daladala ili kuwafikia watu wengi zaidi, ingawa wananchi bado wanalia na gharama kubwa za ununuzi wa majiko ya kisasa.
Kutumia nishati safi ya kupikia ni kampeni ya Serikali inayolenga kupunguza uharibifu wa mazingira na kuepuka madhara yatokanayo na mkaa na kuni wakati wa matumizi ambapo kinara wa kampeni hiyo ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Kampuni ya Pika Smart kwa siku tatu mfululizo inatembelea masoko ya katikati ya Jiji la Dodoma na vituo vya daladala huku wakiwa na ratiba ya kuelekea vijijini katika siku za minada na mikusanyiko ili kuongeza hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Balozi wa Pika Smart Lightness Felix amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka Tanzania isiwe na mtu anayetumia kuni wala mkaa na kwamba hali ilivyo kwa sasa inaonyesha mafanikio makubwa.
Amesema ndani ya kipindi kifupi ambacho wamezunguka katika mikoa mitano, wanaona mwanga mkubwa wa kufikia mafanikio hayo kwani watu wengi wanaojitokeza kupata elimu wamekuwa wakibadili mitazamo na kuanza kutumia majiko ya kisasa.
“Sisi tunazunguka nchi nzima kwa ajili ya kutoa elimu tu, lakini nyuma yetu wapo watu wanaouza majiko sasa tukishatoa elimu tunaona mwitikio wa ununuzi wa majiko ya kisasa unavyokuwa mkubwa tofauti na kama tungewaambia wanunue majiko bila kuwapa elimu kwanza,”amesema Lightness.
Ametaja tatizo la Watanzania wengi kushindwa kuingia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia halitokani na gharama kubwa za majiko bali ukosefu wa elimu ya tofauti kati ya mkaa, kuni, gesi na hata matumizi ya majiko yanayotumia umeme moja kwa moja lakini watu wakishapewa elimu ya tofauti wengi wanakimbilia kwenye mpango wa nishati safi.
Meneja wa Mkoa wa Dodoma katika majiko ya Positive Cooker, Eliud Swai amesema mwitikio wa watu kununua majiko katika ofisi na wakala wao umekuwa mkubwa tofauti na zamani walipoanza.
Swai amesema kiwango cha uelewa kwa wananchi kuhusu majiko yanayopika kwa nishati safi kimeongezeka kwani wanapofika katika vituo vyao kununua majiko huwa hawana sababu za kuuliza jinsi ya kutumia tena.
Hata hivyo amekiri wengi kulalamika kuwa bei ya ununuzi wa majiko hayo bado iko juu jambo linalowanyima fursa ya kununua majiko ingawa wanayatamani lakini akasema bei hiyo ni nafuu zaidi ya mara kumi ukilinganisha na matumizi ya mkaa na kuni.
Margareta Chisinjila kutoka Kijiji cha Mloda amekiri matumizi ya majiko ya kisasa ikiwemo mitungi ya gesi yanatumia muda mchache kupika chakula lakini ni salama zaidi ingawa anakiri kuwa gharama za kuyapata bado ni kubwa.
Margareta amesema bei zinazouzwa vifaa hivyo ziko juu ukilinganisha maisha na kipato cha watu wa vijijini ambao mara nyingi wanapata fedha kwa msimu mmoja wa mazao akashauri kama itabidi Serikali itoe ruzuku au kuwakopesha na wawe wanalipa kidogo kidogo.
“Ukweli ni kuwa, gharama ya kutumia siyo kubwa, lakini wananchi wengi wanaona kuni ziko jirani watoto wanakwenda kuokota halafu atoe Sh50,000 hadi Sh100,000 kununua jiko inakuwa vigumu ingawa hilo litumika muda mrefu na kumrahisishia kupika kwa haraka hasa msimu w akilimo,” amesema Margareta.
Mkulima huyo ameshauri elimu zaidi ipelekwe vijijini siyo kuishi kwenye vituo vya mabasi lakini huduma za mawakala zisogezwe maeneo hadi vijiji ili kuwapunguzia gharama wananchi wakati wa kufanya marekebisho ya majiko ya kujaza gesi.