BENKI ya Equity Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chama cha Watengenezaji wa Bidhaa za Ngozi Tanzania (TALEPPA) kwa lengo la kufungua fursa za minyororo ya thamani katika sekta ya ngozi nchini.
Pia katika makubaliano hayo yameambatana na uzinduzi wa Mradi wa Viatu vya Ngozi vya Shule Tanzania (TALSSI) ambao unalenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi kupitia uzalishaji wa viatu vya wanafunzi.
Makubaliano hayo yamefanyika leo Septemba 2, 2025 Jijini Dar es Salaam, ambapo makubaliano hayo yameshuhudiwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho Manongi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye tukio hilo.
Akizungumza kwenye tukio hilo, Bw. Manongi amewapongeza Benki ya Equity kwa kazi nzuri wanayofanya katika kutoa mikopo kwa wawekezaji wa Kitanzania ili waweze kuwekeza katika uchumi wa viwanda.
Aidha amehamasisha Taasisi za Fedha kwa ujumla waweze kuliangalia eneo la sekta ya ngozi kwa mtazamo mpya uliochanya ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka masharti nafuu zaidi na rafiki kwa viwanda vidogo na vya kati.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Kilimo Biashara kutoka Benki ya Equity, Bi. Teofora Madilu amesema kuwa benki hiyo imejipambanua kwamba wanataka kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya mifugo
“Tumeona kuna thamani kubwa sana kwenye sekta ya mifugo, na thamani hiyo kubwa inawanufaisha watengenezaji wa mwisho wa bidhaa za ngozi kuliko mfugaji ambaye anaishia tu kuuza nyama lakini ile faida kubwa ambayo ni thamani ya ngozi haipati”. Amesema.
Amesema wameanza kufanya kazi na wadau mbalimbali kuanzia Wizara ya Mifugo ili kuhakikisha mifugo inafugwa katika namna ambayo itasababisha upatikanaji wa ngozi bora.
Pamoja na hayo amesema kuwa kama wataweza kuisaidia TALEPPA kwa kuweza kuimarisha viwanda vya ngozi nchini, tuna uhakika mkubwa watakuwa wamechangia kwa kiasi kikubwa kuinua sekta ya mifugo nchini.
Amesema kuna mikopĂ´ ambayo wameiandaa kwaajili ya wafugaji lakini pia wauzaji wa ngozi mbichi ambao nao wanachangamoto zao ambazo wamezipitia na kuzifahamu na kuona ni namna gani wanaweza kufanya.
Amesema benki hiyo ikifanya kazi kwa ushirikiano na TALEPPA wanaweza kutatua changamoto kubwa ya uhaba wa mitaji ambayo inawakumba sekta ya viwanda vya bidhaa za ngozi.
Nae Katibu wa TALEPPA, Bw. Timoth funto amesema Chama hicho kinalenga kutengeneza jozi za viatu vya shule milioni 10 vyenye thamani ya shilingi bilioni 300 kwa mwaka, hatua itakayowezesha sekta ya ngozi nchini kuendelea kukua, kuchangia pakubwa katika uchumi na kutoa ajira kwa watu zaidi ya milioni mbili
Amesema wamelenga soko la wanafunzi kwa kuwa ni rahisi kupenya akiweka wazi kuwa soko la bidhaa za ngozi nchini ni kubwa lakini soko limeendelea kuwa chini.
Hata hivyo Bw. Funto amesema kuwa kutokana na miundombinu hafifu, teknolojia duni, wataalamu wenye ujuzi, sera na mazingira ya Ushindani yasiyo na usawa yamefanya bidhaa za ngozi za Tanzania kutokupenya kwenye soko la ndani na kimataifa
Hata hivyo imewekwa wazi kuwa nchi huingiza bidhaa za ngozi takribani jozi za viatu milioni 54 kila mwaka huku uzalishaji wa bidhaa za ngozi ukiwa chini ya milioni tano kwa mwaka.