Fadlu awatega mastaa Simba | Mwanaspoti

KOCHA wa Simba, Fadlu Davids mjanja sana baada ya kupata uhakika ukuta wa timu hiyo umeimarika zaidi kwa kutua beki wa kati mwingine mpya, Wilson Nangu na kipa wa Taifa Stars, Yakoub Suleiman ametoa kauli inayoonekana kama mtego kwa mastaa.

Kocha huyo amesema anawasubiri wachezaji hao kambini waungane na timu ili ajue namna ya kuwatumia, licha ya kujua uwezo waliouonyesha wakiwa JKT Tanzania na hata Stars.

Simba imemalizana na nyota hao wawili waliokuwa Stars iliyoshiriki fainali za CHAN 2024 zilizoandaliwa kwa ushirikiano wa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda ikiwang’oa kutoka JKT Tanzania iliyowapa ‘thank you’ wiki iliyopita kuonyesha kuwa hawakuwa na maafande hao.

Hata hivyo, juzi kocha Fadlu anayejiandaa kuiongoza kwa msimu wa pili mfululizo katika michuano ya msimu huu wa 2025-2026, amevunja ukimya na kusema anatambua viwango vya juu walivyoonyesha wachezaji hao wapya wakiwa na JKT msimu uliyopita, kitu kinachomwaminisha watafanya vizuri Ligi Kuu inayoanza Septemba 17.

Nangu alimaliza na mabao mawili na asisti mbili, Yakoub akiwa na clean sheets nane, kila mmoja amesaini mkataba mpya wa kuitumikia timu hiyo ya Msimbazi, lakini walikuwa bado hawajajiunga kambini kutokana na jukumu ya timu ya taifa inayojiandaa na mechi za kuwania Fainali za Kombe la Dunia za 2026 ikitarajiwa kucheza mechi mbili – Septemba 5 na 9.

Kutokana na hilo, kocha Fadlu alisema anawasubiri kuwaona kambini aungane nao, pamoja na kutambua uwezo walionao na awaliouonyesha wakiwa JKT Tanzania na hata Taifa Stars.

“Ni wachezaji wazuri kwa kile nilichokiona wamekifanya katika ligi msimu uliyopita, kila mmoja kwa nafasi yake kipa ana umakini wa kuokoa hatari na beki anajitoa na anatumia nguvu,” alisema Fadlu.

“Kuhisiana na wataongeza kitu gani kikosini, kwa sasa siwezi kulizungumzia hilo kwa sababu bado hawajaingia kambini, ningewaona katika mazoezi na wenzao ningekuwa na kitu kikubwa cha kuwaelezea.

“Pamoja na hayo yote ninaamini ni vijana ambao wanajua kipi wanakitafuta katika mpira wa miguu, kwa namna ambavyo walikuwa wanapambana kuhakikisha wanaisaidia timu ya JKT Tanzania kufanya.”

Kauli hiyo ni kama inawataka wachezaji hao wajipange vyema mara watakapotua kambini kwa vile watakuwa na kazi ya kumridhisha kocha huyo ili kumshawishi kupangua kikosi kwa wachezaji waliopo, kwani nyota hao wawili ni kati ya wachezaji ya 10 waliosajiliwa na timu hiyo hadi sasa.

Kusajiliwa kwa Yakoub kunaenda kuziba pengo la Ally Salim anayetakiwa kuondoka na amebakiza mkataba wa miaka mitatu, hivyo alikuwa katika makubaliano ya kumalizana na viongozi wa klabu hiyo.

Yakoub atakwenda kukabiliana na ushindani wa Moussa Camara, aliyemaliza kama  kinara wa clean sheets akiwa na 19 sambamba na Hussein Abel, wakati Nangu nafasi ya beki ya kati anakwenda kushindana na Abdulrazack Hamza, Karaboue Chamou na Rushine de Reuck beki kutoka Sauzi.

Msimu uliopita Simba ilimaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipotea mbele ya RS Berkane ya Morocco, ukuta wa timu hiyo ukiundwa na Camara, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ , Abdulrazaq Hamza na Fondoh Che Malone akisaidiana na Chamou. Malone na Tshabalala wametimika kikosi kwa sasa.

Mabosi wa klabu hiyo juzi usiku walizindua uzi mpya wa msimu wa 2025-2026 katika hafla moja ya kishua iliyohudhuria na wageni mbalimbali wakiwamo vigogo wa klabu hiyo, ikiwa ni mwanzo wa maandalizi ya Wiki ya Simba Day itakayofanyika Septemba 10 kwa  Mkapa.