KOCHA Miguel Gamondi ameanza na sare akiwa na Singida Black Stars kwenye mashindano ya Kombe la Cecafa Kagame dhidi ya Ethiopian Coffee kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Katika mechi hiyo ya kwanza ya kimashindano kwa kocha huyo aliyewahi kuifundisha Yanga, tangu apewa mikoba ya kuongoza kikosi hicho, Singida BS ilionekana kutokuwa na makali katika safu yake ya ushambuliaji.
Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Singida BS ilitengeneza nafasi tatu za wazi huku ikionekana kumtumia zaidi Andrew Phiri ambaye alikuwa akishambulia kutokea pembeni, hata hivyo ilishindwa kuzitumia.
Ethiopian Coffee iliwabidi kucheza pungufu kwa zaidi ya dakika 30 katika kipindi cha pili baada ya kipa wao, Ibrahim Danland kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kudaka mpira akiwa nje ya eneo lake na Singida BS kupewa faulo ambayo hata hivyo iliipotea.
Licha ya Gamondi kufanya mabadiliko kadhaa kwenye safu yake ya ushambuliaji ikiwemo kuingia kwa Elvis Rupia, Ethiopian Coffee ilikuwa imara kutokana na idadi kubwa ya wachezaji ambao walikuwa nyuma hasa baada ya kuwa pungufu.
Ibrahim amekuwa mchezaji wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu katika mashindano haya ya Kombe la Kagame.
Katika mchezo ujao Singida BS itacheza dhidi ya Polisi ya Kenya ambayo imeanza mashindano hayo kwa kishindo baada ya kuichapa Garde-Cotes ya Djibouti mabao 4-0.