Gumzo ahadi za wagombea urais, wadau watahadharisha

Dar es Salaam. Wakati kampeni za wagombea nafasi za urais, ubunge na madiwani, zikipamba moto tangu kuanza kwake Oktoba 28, 2025, sera na ahadi mbalimbali zimeendelea kunadiwa majukwaani licha baadhi ya wagombea kuja na ahadi zinazogonga vichwa vya habari hasa ikiangaliwa utekelezaji wake.

Vyama 17 kati ya 18 vilivyosaini kanuni za maadili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu tayari vimeshasimamisha wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo ya urais wa Tanzania bara na Zanzibar.

Vyama hivyo ni CCM, NLD, AAFP, CUF, TLP, NRA, NCCR-Mageuzi, ACT Wazalendo, CCK, SAU, ADA-TADEA, UMD, UDP, ADC, MAKINI na DP.

Chama pekee kati ya 18 kilichosaini maadili lakini hakijasimamisha mgombea wa urais Zanzibar ni Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kikisema kinakomaa na urais wa Jamhuri ya Muungano.

Kwa upande wa Tanzania Bara, Chama cha ACT-Wazalendo hakishiriki ngazi ya urais kutokana na fomu ya mgombea kutopokelewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC, (Kesi ipo mahakamani) aidha, Chadema kutoshiriki kabisa uchaguzi kutokana na kutosaini Kanuni za maadili ya uchaguzi.

Kote bara na visiwani wagombea wameendelea kumwaga sera zao ambazo kwa namna moja au nyingine zimezua mijadala kwenye jamii ikiwemo mitandaoni.

Wapo baadhi ya wagombea ambao awali wakati wa kurejesha fomu na sasa kwenye kampeni wametoa ahadi kama kuwapatia pesa wananchi kwa ustawi wao, kuanzisha mitambo ya Nyuklia Unguja na Pemba kwa ajili ya uzalishaji wa umeme.

Aidha, intaneti ya bure nchi nzima kuchochea maendeleo ya teknolojia, ubwabwa maeneo ya shule na hospitali, wala rushwa kuchapwa viboko wakiwa wanaonekana mubashara, kusaidia vijana kuoa.

Ahadi hizo ni mbali ya zile zilizozoeleka za maji, barabara za lami, matibabu bure, ajira kwa Watanzania katiba mpya, viwanda pia kilimo ambazo wananchi huzisikia kila kampeni.

Msingi wa hili unatokana na uwepo wa wananchi ambao ni wafuasi wa vyama ambao wao hupigia kura mgombea wa chama chake bila ya kujali ahadi.

Vilevile, wapo wananchi wanaosikiliza ahadi na sera zitokanazo kwenye ilani ya chama husika kisha kufanya maamuzi mgombea yupi anamgusa ili ampigie kura.

Akizungumza leo Jumanne na Mwananchi kwa simu, mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, Kiama Mwaimu amesema katika ulingo wa siasa kila mgombea anatafuta lugha inayofaa ili wamchague apate kura.

“Kwa msingi huo ataeleza maneno ya ukweli wakati mwingine chumvi nyingi ili watu wapate imani wamchague,”amesema.

Amesema wagombea wa upinzani wa chama tawala wanatoa ahadi ambazo hata kabla ya kupata madaraka zinaweza kutafsiriwa kama mzaha.

“Chama kilichopo madrakani wagombea wake kutoa ahadi kunakuwa na uwezekano kwakuwa tayari walishakuwa madarakani, wanajua namna gani ya kufanya kutekeleza,” amesema.

Amesema wengine wanatumia ahadi hizo na wakati mwingine lazima tujiulize wanazungumza hayo kutoka kwenye ilani zao na je kama si hivyo watatekeleza vipi.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana amesema kawaida katika uchaguzi kuna mengi ambayo yanatokea ikiwemo ahadi za namna hiyo huku akisema kimsingi ahadi lazima zitokane na ilani ya chama.

Amesema ilani sio jambo jepesi kwakuwa linahitaji utafiti kwa wananchi kukidhi mahitaji yao nini wanataka hivyo wagombea wanapaswa kujikita zaidi huko kwakuwa wananchi wanaosikiliza wanapima nini kinatekelezeka na nini hakitekelezeki.

“Lazima wananchi tusikilize tuchague chuya na mchele wananchi wa Tanzania wanajua lipi linatekelezeka lipi haliwezekani. Kama haiwezekani basi wananchi tunajua hizi ni porojo hizi kweli. Wagombea kazi yao ni kunadi mambo yaliyopo kwenye chama chako na huwezi kutamka mambo ambayo hatujui kama yanaptikana kwenye chama chako,” amesema.

Mathew Sebastian mkazi wa Dar es Salaam anasema ahadi kubwa zisizo na uchambuzi wa kifedha, kisheria na kimkakati mara nyingi ni mbinu ya kuwavuta wapiga kura kwa hisia.

‘‘Wananchi wanapaswa kuziangalia kwa jicho la ukosoaji na kuuliza maswali ya “inawezekana vipi? kwa gharama gani? kwa muda gani?,” amesema Sebastian.

Mkazi wa Dar es Salaam, James Mozeh amesema kama wagombea wanaotoa ahadi za namna hiyo wanaweza kutekeleza endapo wakipata madaraka basi suala hilo halina tatizo muhimu ni kufanya kile walichoahidi kwasababu yote ni faida kwa watanzania.

Sasha Abdallah anasema baadhi ya ahadi ni ngumu kutekelezeka ikilinganishwa na bajeti husika ya ahadi ya mgombea endapo akipata kiti.