Jamhuri iko freshi, meneja aita mashabiki

Zikiwa zimebaki takriban wiki mbili na ushei kabla ya kurejea kwa Ligi Kuu Bara, Uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Dodoma upo tayari baada ya awali kufungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na matatizo mbalimbali.

Meneja wa uwanja huo, Hussein Muhondo amesema dimba hilo ambalo linatumiwa na Dodoma Jiji limeshafanyiwa marekebisho na kwamba kwa sasa liko tayari kwa ajili ya mikikimikiki ya ligi hiyo.

Machi, mwaka huu, TFF ilivifungia viwanja vitatu ukiwamo wa Jamhuri, CCM Kirumba – Mwanza unaotumiwa na Pamba Jiji na Liti uliopo Singida unaotumiwa na Singida Black Stars.

Akizungumza na Mwanaspoti, Muhondo alisema baada ya rungu la kufungiwa kutokana na kutokidhi baadhi ya vigezo ikiwemo sehemu ya kuchezea, hivi sasa umerekebishwa na hivi majuzi maofisa wa TFF walikwenda kuukagua na kuufungulia isipokuwa waliwataka wamiliki warekebishe eneo la kukaa wachezaji wanaokuwa benchi.

“Sehemu ya kuchezea bado inaendelea kuboreshwa zaidi. TFF walikuja kukagua tuliambiwa turekebishe mabenchi ya wachezaji tu na sehemu zingine zote ziko sawa. Mashabiki wasiwe na wasiwasi, wajitokeze kwa wingi mechi yetu na Coastal Union Septemba 27, mwaka huu, hapahapa Jamhuri Dodoma,” alisema.

Mwanaspoti lilijionea uwanja huo ambao umewekewa mfumo wa kumwagilia maji na pia mistari ya alama bado inang’ara ikiufanya uonekane vizuri. Pia umeboreshewa mfumo wa mifereji ya maji ili mvua inaponyesha usituamishe maji kirahisi na kusababisha tope pale mechi zinapochezwa.

Gazeti hili pia limeshuhudia vyoo vya mashabiki vikiwa na mifumo mipya ya kisasa, safi na vyenye maji pamoja na maeneo ya kuoshea mikono, vyumba vya kubadilishia nguo timu.

Sehemu inayoonekana kuwa na changamoto ni mageti ya kuingia ndani ya uwanja na pia mabenchi ya wachezaji yanaonekana kuchoka na hayana uimara.