Mahakama yabariki kifungo cha miaka 30 kwa waliohukumiwa kwa kuiba kaboni ya dhahabu

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Musoma imebariki adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa Maneno Chanila na Joseph Daud, waliokutwa na hatia ya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba kaboni ya dhahabu yenye thamani ya Sh109 milioni.

Kumbukumbu za mahakama zinaonesha kuwa wawili hao na wenzao wanne (si warufani katika rufaa hiyo) walitenda kosa hilo Aprili 7, 2024, katika Kijiji cha Magunga, wilayani Butiama mkoani Mara.

Maneno na mwenzake, ambaye pia ni maarufu kwa jina la Profesa, walikutwa na hatia na kuhukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Butiama.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Marlin Komba, Agosti 29, 2025, aliyekuwa akisikiliza rufaa iliyokatwa na Maneno na mwenzake wakipinga adhabu hiyo.

Jaji Komba amesema, baada ya kupitia mwenendo, sababu za rufaa na hoja za mjibu rufaa, anatupilia mbali rufaa hiyo kwani haina mashiko na kwamba utetezi wa warufani haukutikisa ushahidi wa upande wa mashtaka na adhabu waliyohukumiwa si kali ikilinganishwa na ilivyotolewa chini ya kifungu maalumu.

Warufani hao walitiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na makosa mawili, kinyume na kifungu cha 287A cha Kanuni ya Adhabu.

Wakiwa na wenzao wanne waliiba kaboni hiyo mali ya Patrick Ryoba na, baada ya kuiba, walitumia panga kumjeruhi Joh ambapo pia waliiba fedha Sh85,000, simu tatu za mkononi mali ya Chacha Wambura, na kabla hawajamuibia walitumia panga kumjeruhi mtu huyo ili kupata mali hizo.

Katika rufaa hiyo, warufani hao walikuwa na sababu saba za rufaa, ambazo ni pamoja na kudai kuwa Mahakama ilikosea kisheria kuwatia hatiani kwa kosa la wizi wa kutumia silaha bila ushahidi wa kutosha na wa kuaminika uliowaunganisha moja kwa moja na kosa hilo.

Nyingine ni kuwa Mahakama ilikosea kutegemea maelezo yao ya onyo yaliyokubaliwa katika ushahidi licha ya kutokuwa na uthibitisho na bila kufanya uchunguzi sahihi.

Sababu nyingine ni kuwa mashahidi wa mashtaka, hasa shahidi wa nane na wa 13, walitoa ushahidi wao kwa kuzingatia vielelezo na maelezo yao ya onyo ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na wao, ikiwa ni pamoja na gari linalodaiwa kutumika katika wizi huo, ambalo halikuhusishwa na warufani kwa umiliki.

Nyingine ni kuwa hukumu hiyo ilitokana na mazingira ya ushahidi wa kubahatisha badala ya ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha bila shaka yoyote kuwa warufani walishiriki kosa hilo. Pia, Hakimu alishindwa kuzingatia kesi ya utetezi.

Wakati wa usikilizaji huo, warufani hao walijiwakilisha mahakamani wenyewe bila uwakilishi wa wakili, huku mjibu rufaa (Jamhuri) akiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Beatrice Mgumba, ambaye alipinga rufaa hiyo huku warufani hao wakiiomba Mahakama iwaone hawana hatia.

Miongoni mwa hoja za wakili wa mjibu maombi ni pamoja na sababu ya utetezi wa warufani kutochambuliwa, ambapo aliiomba Mahakama Kuu kutekeleza jukumu la Mahakama ya chini kwa kuchambua utetezi kama ilivyoamuliwa katika moja ya kesi za rufaa.

Wakili huyo aliikumbusha Mahakama kuwa warufani walishtakiwa kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na kuwa adhabu iliyotolewa ilitolewa chini ya kifungu husika ambacho kinaelekeza adhabu inapaswa isipungue kifungo cha miaka 30, na kuiomba Mahakama ione sababu hiyo ni ndogo.

Kuhusu ushahidi wa shahidi wa nane na wa 13, wakili huyo aliieleza Mahakama kuwa mashahidi hao ndiyo chanzo cha kukamatwa kwa warufani na kwamba shahidi wa nane alikuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Butiama, ambapo ndipo uhalifu ulipofanyika.

Wakili huyo alichambua sehemu ya ushahidi wa shahidi huyo ambaye alieleza kupata taarifa kutoka kwa mtu mmoja kuhusu alipo mrufani wa kwanza, ambaye baada ya kukamatwa alikiri kuhusika na wizi huo wa kutumia silaha ambapo aliwataja watu wengine, akiwemo mrufani wa pili na Eze.

Alieleza kuwa, katika kumtafuta Eze, gari moja lilikamatwa na kukutwa na chembechembe za kaboni, kisha kuwaunganisha warufani na uhalifu huo uliotokea katika kiwanda cha dhahabu.

Wakili huyo alieleza kuwa shahidi wa 13, wakiwa wanarekodi maelezo ya onyo, warufani walieleza kuhusu gari hilo ambalo lilikamatwa na kwamba kukiri kwa hiari kwa mshtakiwa ni ushahidi bora, na katika rufaa iliyopo warufani walikiri na kueleza jinsi walivyotumia gari kutekeleza uhalifu.

Wakili huyo alieleza kuwa uhusiano wa warufani na tukio hilo upo kwenye kielelezo cha 25, ambacho ni ripoti ya sampuli za vinasaba (DNA) ambayo inalingana na sampuli iliyochukuliwa kutoka kwa mrufani wa pili, aliyekuwa amejeruhiwa katika eneo la tukio na kutumia nguo kupaka damu.

Wakili huyo alihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa wizi wa kaboni kwenye kiwanda hicho ulifanywa na warufani.

Jaji Komba amesema, baada ya kupitia mwenendo, sababu za rufaa na hoja za mjibu rufaa, ataanza kwa kuainisha kuwa katika kesi za jinai, upande wa mashtaka una wajibu wa kuthibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa kama inavyoelezwa katika kifungu cha 3(2) cha Sheria ya Ushahidi.

Jaji amesema, katika rufaa hiyo, upande wa mashtaka haukuwa na ushahidi wa macho na kwamba katika kesi ya msingi, upande wa mashtaka ulitegemea ushahidi wa kimazingira na au maelezo ya onyo ikiwa yapo.

Akipitia sababu hizo, Jaji amesema kuhusu utetezi wa warufani kutochambuliwa na kutozingatiwa na Mahakama ya chini, amepata muda wa kusoma utetezi wa warufani na kuhitimisha kuwa utetezi wao haukutikisa kesi ya mashtaka.

Amesema rekodi inaonesha kuwa kaboni hiyo iliibiwa na warufani hao na mtu mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Eze, na kwa kuwa hiyo ni rufaa ya kwanza, Mahakama ina mamlaka ya kuchambua utetezi na baada ya uchambuzi ameona upande wa utetezi haukutikisa kesi ya mashtaka.

“Kuhusu adhabu, warufani walihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela. Nilisoma sheria chini ya kifungu cha 287A ya Kanuni ya Adhabu, ambayo imetaja muda wa chini wa kifungo.

“Kwa kusoma kesi iliyopo na ushahidi uliopo, warufani walitakiwa kuadhibiwa kwa kosa hilo na hukumu iliyotolewa si kali ikilinganishwa na ilivyotolewa chini ya kifungu maalumu. Kwa ujumla, naona rufaa haina mashiko na ninaitupilia mbali,” amehitimisha Jaji.