Mahakama yaridhia Exim kumshtaki Gavana BoT

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeiruhusu Benki ya Exim kufungua shauri dhidi ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupinga uamuzi wa kuirejeshea isivyo halali Kampuni ya Swiftline Logistics Limited Dola 224,000 za Marekani zilizochukuliwa kwenye akaunti.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Awamu Mbagwa, katika shauri la Exim la kuomba kibali cha kufungua maombi ya mapitio kupinga uamuzi wa Gavana.

Kampuni ya Swiftline Oktoba 17, 2024 iliwasilisha malalamiko kwa Dawati la Usuluhishi wa Migogoro BoT, lililoanzishwa kwa ajili ya kusuluhisha malalamiko ya wateja wa huduma za kifedha dhidi ya watoa huduma hizo.

Ilidai Exim iliidhinisha kwa njia isiyo halali utolewaji wa Dola 224,000 (zaidi ya Sh549 milioni kwa kiwango cha ubadilishaji fedha cha BoT) kutoka kwenye akaunti yake.

Dawati hilo katika uamuzi wa Oktoba mosi, 2024, pamoja na mambo mengine, liliiamuru benki kuirejeshea kampuni fedha hizo.

Benki haikuridhika na uamuzi huo ikafungua shauri la marejeo kwa Gavana.

Gavana katika uamuzi wa Novemba 27, 2024 alikubaliana na uamuzi wa dawati.

Exim haikuridhika ikafungua shauri la maombi dhidi ya Gavana wa BoT, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kampuni ya Swiftline, kama mdaawa muhimu katika shauri hilo, ikiomba kibali kuupinga mahakamani uamuzi wa Gavana, ombi ambalo limekubaliwa.

Jaji Mbagwa katika uamuzi alioutoa Agosti 29, 2025, amesema baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na mwombaji kwa njia ya maandishi, kiapo cha Mkuu wa Idara ya Sheria wa mwombaji, Edmund Mwasaga, maelezo na vielelezo, amebaini amekidhi vigezo, ambavyo ni shauri kufunguliwa ndani ya miezi sita tangu kutolewa uamuzi unaokusudiwa kupingwa.

Vilevile, mwombaji kuonyesha kuna hoja inayobishaniwa inayostahili kuamuliwa na mwombaji kuonyesha kuwa ana masilahi ya moja kwa moja katika jambo linalobishaniwa.

Akizungumzia muda, Jaji Mbagwa amesema uamuzi unaopingwa ulitolewa Novemba 27, 2024 mwombaji alifungua shauri Desemba 23, 2024, siku 26 baada ya uamuzi huo.

Kuhusu hoja inayobishaniwa Jaji Mbagwa amesema katika aya ya saba ya maelezo ya mwombaji yanayounga mkono shauri hilo, ameibua masuala kadhaa, uamuzi wa dawati la usuluhishi la BoT na athari zake.

Pia, tafsiri sahihi ya mamlaka ya akaunti, usahihi wa amri ya kurejesha fedha, kikomo cha muda kinachohusiana na uamuzi wa dawati na matumizi yasiyo sahihi ya vifungu vya sheria.

“Bila kuingia kwa kina katika hoja hizo, nimeridhika kwamba kwa madhumuni ya kutoa kibali, ukweli ulioelezwa unaonyesha kuwapo hoja ya msingi,” amesema.

Iwapo mwombaji amethibitisha kuwa na masilahi ya kutosha katika shauri hili, Jaji Mbagwa amesema hakuna ubishi kwamba uamuzi wa mjibu maombi wa kwanza (Gavana) ulimwathiri mwombaji.

Amesema katika uamuzi huo,  mwombaji ndiye aliamuriwa  kumrudishia Swifline Dola 224,000.00 na kwamba, hiyo inaonyesha namna mwombaji alivyoathirika moja kwa moja na uamuzi huo, hivyo kuthibitisha masilahi ya kutosha ya mwombaji katika shauri hilo.

“Baada ya kuzingatia yote hayo, ninafikia hitimisho lisilo na shaka kwamba maombi haya yana mashiko. Kwa hiyo, kibali kinatolewa kwa mwombaji kuomba mapitio ya mahakama kwa amri ya kufuta uamuzi wa Gavana wa BoT,” amesema.

Amesema kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga uamuzi wa Gavana, kinatumika pia kama amri ya kusitisha utekelezaji na/au uhalalishaji wa uamuzi wa Gavana hadi shauri hilo la mapitio ya mahakama litakapoamuliwa.

Benki hiyo katika shauri hilo iliomba kibali cha kuomba amri ya kufuta uamuzi wa Gavana au kwa njia mbadala, amri za kumlazimisha Gavana kutupilia mbali malalamiko ya Swifline kuwa hayana mashiko.

Amri mbadala ni kumlazimisha Gavana awaamuru wahusika wengine katika akaunti hiyo waliohusika wazirudishe na pia kibali hicho kitumike kama amri ya zuo la utekelezaji wa uamuzi wa Gavana mpaka shauri tarajiwa la mapitio litakapoamuliwa.

Gavana na AG kupitia majibu yao ya maandishi na kiapo kinzani kilichoapwa na Wakili wa Serikali Erigh Rumisha na Swiftline katika kiapo kinzani cha Mkurugenzi Mtendaji wake, Julius Mugarangu, walilipinga shauri hilo.

Shauri hilo lilisikilizwa kwa maandishi upande mmoja, kutokana na Gavana na AG kushindwa kuwasilisha maelezo ya utetezi wao huku, Swiftline kupitia barua ya Aprili 14, 2025, iliijulisha Mahakama kwamba, baada ya kutafakari haikuona sababu ya kupinga maombi hayo.