Manyika aingia Namungo na mkakati wa kufuta rekodi mbovu

Rekodi ya Namungo kuwa na wastani wa kuruhusu mabao 30+ katika kila msimu ndani ya misimu sita iliyoshiriki Ligi Kuu Bara tangu 2019-2020, imemfanya kocha wa makipa wa kikosi hicho, Peter Manyika, kuingia na mpango kazi maalum.

Manyika amesema katika kuhakikisha lango la timu hiyo linakuwa salama zaidi, anapambana kuwaandaa vijana wake kuwa katika kiwango sawa chenye ubora.

Manyika anasema anafanya hivyo ili siku ikitokea yule ambaye ni chaguo la kwanza anakosekana, basi kusiwe na tofauti atakayechukua nafasi yake. Makipa wa Namungo kuelekea msimu wa 2025-2026 ni Jonathan Nahimana, Lucas Chembeja, Mussa Malika Mussa na Suleiman Said Abraham.

Kocha huyo ametua Namungo hivi karibuni baada ya msimu uliopita kuwa kwenye benchi la ufundi la Dodoma Jiji, timu iliyoruhusu mabao 49 katika mechi 30 za Ligi Kuu Bara.

Takwimu zinaonesha kuwa, Namungo ambayo tayari imeshiriki misimu sita ndani ya Ligi Kuu Bara, imekuwa na wastani wa kuruhusu mabao 30+ kila msimu jambo ambalo ni hatari kwa timu yenye malengo makubwa.

Ni msimu mmoja pekee iliruhusu mabao chini ya 30 japo ilikaribia kufikia idadi hiyo, ilikuwa 2023-2024 ambapo nyavu zake zilitikiswa mara 29.

Misimu mingine ilikuwa hivi; 2019-2020 (iliruhusu mabao 37), 2020-2021 (iliruhusu mabao 31), 2021-2022 (iliruhusu mabao 34), 2022-2023 (iliruhusu mabao 33) na 2024-2025 (iliruhusu mabao 36).