KOCHA Mkuu wa KMC, Marcio Maximo amesema uwepo wa timu hiyo katika michuano ya Kombe la Kagame 2025 itakuwa chachu katika kufanya maandalizi bora ya msimu 2025/26 kutokana na kukutana na timu ngumu zinazoshiriki michuano ya kimataifa.
KMC na Singida Black Stars zimepata nafasi ya kushiriki michuano hiyo baada ya Simba na Yanga kujiengua kutokana na ratiba kuzibana zikijiandaa na michuano ya ndani na kimataifa.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema michuano hiyo itatoa picha nzuri ya ubora wa kikosi chao kwani wanakwenda kushindana na timu zenye ubora na uzoefu kwenye ligi zao.
“Nimefurahia nafasi tuliyoipata ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi tunakwenda kushindana malengo ni kufanya vizuri na kujiweka tayari kwa ligi kuu,” alisema kocha huyo Mbrazili:
“Wachezaji wangu wapo tayari kwa kushindana maandalizi tuliyoyafanya yatafanywa kwa vitendo kwa kucheza mechi za ushindani kabla ya ligi kuanza.”
Akizungumzia ratiba ya ligi, Maximo alisema ameiona na atatambua anaanza na timu ya aina gani furaha kwake ni kuanza kwenye uwanja wa nyumbani na wachezaji wake kuwa na utayari baada ya maandalizi ya muda.
“Baada ya kuona ratiba tulikaa na timu na kuzungumza ni namna gani tunatakiwa kufanya kubwa ni kuhakikisha tunaanza vizuri tukiwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani lakini pia kumheshimu mpinzani,” alisema. KMC itaanza msimu mpya kwa kuvaana na Dodoma Jiji Septemba 17 kwenye mechi ya kwanza ya ufunguzi wa ligi kuu bara huku Coastal Union ikiwa nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons.