MSHAMBULIAJI wa Dodoma Jiji, Yassin Mgaza, ameendeleza moto wa kucheka na nyavu katika mashindano ya Tanzanite Pre-Season International baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Coastal Union.
Mgaza ambaye amefikisha mabao matatu na kuwa kinara wa ufungaji kwenye michuano hiyo, alianza kuziona nyavu za Coastal Union mapema tu dakika ya pili akiitumia vizuri pasi ya William Edgar.
Ubora wa safu ya ushambuliaji ya Dodoma Jiji, ulileta matunda mengine dakika ya 11 kupitia Mgaza aliyefunga bao la pili pia akitumia vizuri pasi ya Edgar.
Kuingia kwa mabao hayo chini ya dakika 15 za kwanza, zililishtua benchi la ufundi la Coastal Union chini ya Kocha Ali Mohamed.
Hata hivyo, Coastal ilijibu mapigo dakika ya 15, lakini shuti kali la Cleophace Mkandala akiwa nje ya 18, vipimo vilizidi kidogo, mpira ukagonga mlingoti na kurudi uwanjani.
Dakika ya 26, benchi la ufundi la Coastal Union lililazimika kufanya mabadiliko ya mapema upande wa winga ya kushoto kwa kumtoa Ezekiel Dhaifu na kuingia Pius Peter.
Muda mfupi baada ya mabadiliko hayo, Dodoma Jiji ikaongeza bao la tatu dakika ya 29, mfungaji akiwa Jofrey Kasanga ambaye alimalizia mpira uliokuwa ukizagaa karibu na lango la Coastal Union kufuatia shuti la Mgaza kuzuiliwa.
Coastal Union ilipambana kuhakikisha haiendi mapumziko kichwa chini kufuatia Athuman Masumbuko kufunga bao kwa kichwa dakika ya 40, akiunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Kiala Lassa. Mapumziko ikawa Dodoma Jiji 3-1 Coastal Union.
Ziliporejea kipindi cha pili, timu zote zilikuwa imara, hakuna aliyekubali unyonge hali iliyofanya safu zao za ulinzi kulinda vizuri nyavu zao hadi mwisho ubao ukabaki ukisoma Dodoma Jiji 3-1 Coastal Union.
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa Coastal Union katika michuano hii inayofanyika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara ikishirikisha timu 10 zilizopangwa makundi matatu.
Kwa Dodoma Jiji, ulikuwa mchezo wa pili baada ya ule wa kwanza dhidi ya Tanzania Prisons kutoka sare ya bao 1-1 ambapo Mgaza aliisawazishia Dodoma Jiji kwa penalti dakika ya 90+4.
Kundi B lenye timu tatu, kwa sasa linaongozwa na Dodoma Jiji yenye pointi nne baada ya kucheza mechi mbili, inafuatia Tanzania Prisons iliyokusanya pointi moja katika mechi moja, huku Coastal Union haina kitu nayo ikishuka dimbani mara moja.
Dodoma Jiji ikiwa imemaliza mechi zake hatua ya makundi, inaiombea Tanzania Prisons mchezo wa mwisho dhidi ya Coastal Union ipoteza au ipate hata sare, yenyewe ifuzu nusu fainali kwani kundi hilo linatoa timu kinara kucheza hatua inayofuata kuungana na Tabora United iliyotangulia kutoka Kundi A.
Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yanayofanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, yakiandaliwa na Fountain Gate FC, yalianza Agosti 31, 2025 na tamati yake ni Septemba 7, 2025 ambapo utapigwa mchezo wa fainali. Kabla ya hapo, Septemba 6, zitachezwa mechi za nusu fainali.
Jumla ya timu 10 zinashiriki zikiwa zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A lina timu za Fountain Gate, Tabora United na Eagle FC ya Manyara.
Kundi B zipo Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union, huku Kundi C kuna Namungo, JKU ya Zanzibar, City Abuja (Nigeria) na TDS inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa inaibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.
Kesho Septemba 3, 2025, ratiba inaonesha Namungo itacheza dhidi ya TDS saa 7:00 mchana, kisha saa 10:00 ni City FC Abuja dhidi ya JKU.