Morogoro. Mgombea mwenza urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja amewahakikishia Watanzania endapo chama hicho kitaingia madarakani kero ya tozo za mazao ya kilimo na utitiri wa kodi kwa wafanyabiashara zitaondolewa.
Amesema Serikali ilipaswa kuwawezesha wakulima kwa zana bora za kilimo na sio kusubiri wakulima kuteseka kulima, kuvuna na baadae kudaiwa ushuru.
Kwa upande wa kodi,amesema wafanyabiashara wanapitia mateso kwa kufungiwa biashara zao sababu ya kodi zisizo rafiki huku wafanyabiashara wakubwa wakisamehewa kodi, jambo ambalo amesema suluhu ni kukichagua chama hicho kiunde Serikali kuondoa matatizo hayo.
Mgombea huyo ametoa kauli hiyo leo Septemba 2, 2025 wakati akizungunza na wananchi wa Jimbo la Kilombero ukiwa ni mwanzo wa kampeni yake katika mkoa huo kuwaeleza wananchi sababu ya kukichagua chama hicho kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu
“Wananchi wa Ifakara mnalima mpunga, hapa naambiwa kila gunia ni Sh5,000 ushuru, hivi kweli unahangaika jua lako, mbolea, dawa na kufukuza ndege shambani, alafu ukivuna mazao yako unakutana na geti la ushuru, uonevu gani huu chini ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ndugu zangu hawa tuwakatae,” amesema.
Amesema uwepo wa ushuru usio rafiki kwenye mazao ya kilimo, ni matokeo ya Serikali kushindwa kufikiria njia bora za mapato zisizo na muumiza mkulima.
Devotha amesema pamoja na miundombinu ya barabara kuwa mibovu kila pahala ndani ya mkoa huo yapo mageti mahususi kuzuia wakulima kuwadai ushuru wa mazao wanayoteseka kulima.
Akizungumzia wafanyabiashara, Devotha amesema kumekuwa na matumizi makubwa ya nguvu wakati wa ukusanyaji kodi hali inayowalazimu wafanyabiashara kufunga maduka yao.
“Wafanyabiashara wanafunga biashara zao kwasababu ya kodi kubwa, mtu unafungua biashara mtaji Sh1 milioni anakutana na mrundikano wa kodi, mfanyabiashara huyu atapumuaje, lazima Serikali iwasaidie wafanyabiashara hawa.”
“Chauma ikiingia madarakani lazima tutaanza kurekebisha mifumo ya kodi, tuwe na kodi rafiki, tutakuwa na mwaka mmoja kwa wafanyabiashara wanaoanza biashara tukiangalia mapato yao na baishara zao tujue wanachopata ndipo tuwalipishe kodi,” amesema mgombea mwenza huyo.
Amesema ni jambo la ajabu wafanyabiashara wakubwa kusamehewa kodi wakati wapo wafanyabiashara ndogondogo wanafunga biashara kutokana na utitiri wa kodi.
Amesisitiza kuwa Chaumma kikiaminiwa na Watanzania kuunda Serikali wafanyabiashara wakubwa hawawezi kusamehewa kodi na nguvu itawekwa kwa kundi hilo kupata mapato.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Kilombero kwa tiketi ya Chaumma, Magreth Raphael amesisitiza kero ya wakulima kutozwa Sh5,000 kwa kila gunia la mazao akisema umeanzishwa utaratibu wa kushusha magunia kwenye gari na kuhesabu.
“Mpunga unashushwa kwenye gari na kuhesabiwa kulipa ushuru na baadae magari kutozwa fedha za maegesho, hili sio sawa tunawaomba Watanzania ntuchague tukawaletee mabadiliko,” amesema.