Musoma. Mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Gombo na mgombea mwenza wake, Husna Abdallah wameshindwa kufika katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliopangwa kufanyika mjini Musoma kutokana na changamoto za barabara.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mgombea huyo alitarajiwa kufanya mkutano huo leo, Agosti 2, 2025, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo, uliopo katikati ya Manispaa ya Musoma.
Awali, gari la matangazo lilipita mitaani likitangaza kwamba mgombea huyo angewahutubia wananchi kuanzia saa nane mchana, kabla ya muda huo kubadilishwa na kutangazwa upya kuwa mkutano ungefanyika saa kumi jioni.
Msemaji wa kampeni za CUF, Lutalosa Yemba akizungumza na Mwananchi, amesema msafara wa wagombea wao ulipata matatizo makubwa kutokana na wingi wa vumbi barabarani walipokuwa wakielekea Musoma Vijijini kwa ajili ya mikutano ya kampeni.
“Mimi si msemaji wa afya ya mgombea, ila ninachoweza kusema ni kwamba wengi tuliokuwa kwenye msafara tumepata madhara makubwa. Watu wana mafua makali, hata mimi najikaza kuzungumza,” amesema Yemba.
Amesema baada ya kumaliza mkutano Bunda jana, walielekea Musoma Vijijini leo asubuhi. Wakiwa njiani wamelazimika mara kwa mara kushuka kwenye magari kuzungumza na wananchi waliokuwa wakijitokeza, hali iliyowasababishia madhara ya vumbi kutokana na barabara duni.
“Hali hii imesababishwa na Serikali ya CCM kwa kushindwa kujenga barabara za lami. Hata hivyo, hatutumii hili kama kisingizio. Nimeamua kufika ili mkutano uendelee hata kama mgombea wetu hayupo, naamini wananchi wametuelewa kwa maelezo tuliyoyatoa,” amesema Yemba.
Hadi sasa haijajulikana iwapo mgombea huyo ataendelea na ratiba ya kampeni au la.
Ahadi za kuboresha huduma
Katika mkutano huo, mgombea ubunge wa CUF jimbo la Musoma Mjini, Omari Mohamed akiwahutubia wananchi, ameahidi kushughulikia kero za wananchi, hususan wajawazito.
“Ni jambo la kusikitisha kuona akinamama wajawazito wakielekea hospitalini kujifungua wakiwa wamebeba mabeseni na mabegi, hali inayofanya waonekane kana kwamba wanahamia nyumba ya jirani. Nikichaguliwa, nitaifanyia kazi kero hii kwa kuhakikisha akinamama wanahudumiwa ipasavyo,” amesema.
Ameahidi iwapo Wizara ya Afya haitaboresha huduma za afya, atakuwa anatumia fedha zake binafsi kusaidia kuboresha mazingira ya kujifungulia.
“Mimi siendi bungeni kwa ajili ya maslahi binafsi, nakwenda kuwawakilisha wananchi wa Musoma. Akina mama watakapohitaji kujifungua watapiga simu na ‘ambulance’ itawafuata majumbani,” ameongeza.
Hoja kuhusu usawa wa kisiasa
Ofisa Masijala wa CUF, Imani Nassoro amesema chama hicho kimeingia kwenye uchaguzi kikiwa na matarajio ya kuona Tume ya Uchaguzi inatenda haki bila upendeleo.
“Tunataka kujua kama kweli tume hii ni huru kama inavyodai, au ni jina tu. Hili litaonekana kupitia namna watakavyosimamia mchakato wa uchaguzi,” amesema.
Ameongeza kuwa mazingira ya kisiasa yamekuwa magumu kwa vyama vya upinzani kupata wagombea kutokana na hofu ya kushughulikiwa na vyombo vya dola, ikiwemo kufilisiwa, hali inayowalazimisha baadhi kuunga mkono chama tawala bila hiari.
“Sote tumeshuhudia viongozi wa serikali na wa polisi wakiteuliwa kuwa wakuu wa mikoa au kushika nyadhifa ndani ya CCM. Hili linaonyesha namna nchi yetu inavyoendeshwa kinyume na utaratibu,” amesema kiongozi huyo alipokuwa akiwanadi wagombea wa nafasi za udiwani ubunge wa chama chake.
Aakizungumzia sera ya CUF, Nassoro amesema imeamua kuja na haki sawa kwa wote, ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali za nchi.
“Kipato cha msingi ni haki ya kila Mtanzania. Maeneo yenye fursa tutayabinafsisha ili kuweka mifumo bora ya kuhakikisha kila mmoja ananufaika, kwa sababu hadi sasa wananchi hawajapata neema yoyote,” amesema.