Miili ya watoto wachanga yaokotwa Dar na Geita, mmoja wachomwa moto

Dar/Geita. Miili ya watoto wachanga wawili imeokotwa katika mazingira tofauti jijini Dar es Salaam na mkoani Geita, mmoja wao ukiwa umetupwa kichakani na kuchomwa moto.

Katika tukio la jijini Dar es Salaam, mwili wa mtoto mchanga wa kiume umeokotwa katika Mtaa wa Mpakani, Kata ya Ndugumbi, Wilaya ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam, baada ya kukutwa ndani ya mfuko wa sandarusi uliokuwa umetupwa karibu na mfereji wa maji machafu.

Tukio hilo limetokea asubuhi ya Septemba 2, 2025, na mashuhuda wamesema mtoto huyo alionekana baada ya mbwa kuanza kubweka huku akizunguka mfuko huo.

Kwa mujibu wa mashuhuda, mmiliki wa mbwa alishtushwa na kelele hizo na alipofungua mfuko, alikutana na mwili wa mtoto huyo akiwa ametapakaa damu huku kondo la uzazi likiwa halijaondolewa.

Tukio hilo ni mfululizo wa matukio ya kutupwa kwa watoto wachanga yaliyotokea hivi karibuni Jijini Dar es Salaam. Agosti 5, 2025, katika Daraja la Tabata Matumbi, mwili wa mtoto mchanga uliokotwa ukiwa kwenye mfuko.

Akizungumza na Mwananchi leo, Septemba 2, 2025 Mjumbe wa nyumba kumi wa mtaa huo, Amisa Mapunda, amesema alipata taarifa za tukio hilo baada ya kusikia kelele za watu waliokusanyika eneo la tukio.

“Nilikuta mtoto mchanga akiwa amefariki dunia, ndani ya mfuko wa sandarusi na kufunikwa kwa kipande cha gauni (dela),” amesema Amisa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mpakani, Kumbukeni Kitembo, amesema alipata taarifa hiyo saa 1:45 asubuhi kutoka kwa mwenyekiti mwenzake wa Mtaa wa Muungano, aliyempigia simu akimjulisha juu ya mtoto mchanga aliyeonekana eneo la mtaa wake.

“Baada ya kupokea taarifa, nilitoa maelekezo kwa sungusungu kufika eneo hilo. Nilipofika, nikakuta mwili wa kichanga wa kiume, kisha nikawasiliana na Jeshi la Polisi ambao walifika na kuuchukua mwili kwa uchunguzi zaidi,” amesema Kitembo.

Kitembo ameongeza kuwa juhudi za kumtafuta mtu aliyetelekeza kichanga hicho zinaendelea, na kwamba kipande cha gauni kilichotumika kufunika mtoto ni miongoni mwa sare za sherehe zilizowahi kutumika mtaani hapo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Muungano, Jane Mndewa, amesema yeye ndiye aliyefika kwanza eneo la tukio baada ya kupokea simu kutoka kwa wananchi wake walioguswa na kilichotokea.

“Nilikuta mfuko ukiwa wazi na ndani yake mtoto mchanga wa kiume akiwa ameshafariki. Alikuwa bado na kondo la uzazi, jambo linaloashiria kuwa huenda alizaliwa na kutupwa muda mfupi baada ya kuzaliwa,” amesema Jane.

Jane amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola ili kufanikisha kukamatwa kwa mhusika wa tukio hilo la kikatili, huku akisisitiza kuachana na matendo ya unyama dhidi ya watoto wasiokuwa na hatia.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema wamepokea taarifa hiyo kutoka kwa wananchi na kufika eneo la tukio mara moja.

“Ni kweli, tumepokea taarifa kuhusu kupatikana kwa kichanga kilichotupwa. Tumekichukua kwa uchunguzi wa kina ili kubaini aliyefanya kitendo hicho,” amesema Muliro.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kutupa watoto, akisisitiza kuwa kuzaa sio kosa na kulea mtoto ni jukumu la wote.

Nako mkoani Geita, mwili wa mtoto mchanga pia wa kiume umekutwa ukiwa umetupwa kichakani na kuchomwa moto katika Mtaa wa Mwatulole, Kata ya Buhalala, Manispaa ya Geita.

Tukio hilo limebainika Septemba mosi, 2025, wakati wananchi walipokuwa wakifanya usafi wa mazingira kwa maandalizi ya kupokea Mwenge wa Uhuru.

Inaelezwa wananchi walipokuta eneo hilo linawaka moto, walipokwenda  kuuzima  ndipo walipoona kitu kinachofanana na mwili wa mtoto.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Geita, Hamis Dawa, amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mtoto huyo anakadiriwa kuwa na umri wa siku moja, alitupwa eneo hilo, kisha kuchomwa moto.

“Bado hatujajua mtoto ni wa nani, tunachunguza kama alitupwa kisha moto ukawashwa au moto uliomfichua,” amesema Dawa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wamelaani kitendo hicho na kusema tukio la unyama lisilo na utu.

Happiness Samuel, mkazi wa Mwatulole, amesema akiwa jirani kwenye msiba alipigiwa simu na kijana wake akielezwa kuna moto umewashwa kwenye shamba lao karibu na mti wa mwembe na kumtaka auzime.

Amesema alipofika eneo la tukio kusaidia kuzima moto, akisaidiana na wananchi waliokuwa wakifanya usafi kwa ajili ya maandalizi ya Mwenge wa Uhuru  na ndipo walipobaini uwepo wa mwili wa kichanga hicho.

“Baada ya kukuta tukio hilo tulimpigia mtendaji simu alifika na kuangalia mwili na kujiridhisha kuwa ni wa binadamu ndipo akapiga simu polisi ambao walifika na kuuchukua mwili kwa uchunguzi zaiid,”amesema  Happiness.

Mwajuma Haruna, mkazi wa eneo hilo, amesema tukio hilo limewaumiza na kuwaomba wananchi kutoa taarifa iwapo wanamfahamu mtu aliyejificha au mjamzito ambaye sasa hana mimba.

“Huu ni unyama mkubwa. Mtu unabeba mimba kisha unaamua kuua na kumchoma moto mtoto? Bora angemuweka hata mlangoni au kwenye nyumba za ibada angepata wa kumlea, sio kumuua kinyama kiasi hiki,” amesema Haruna.

Kamanda Dawa ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kumtambua mhusika wa tukio hilo ili kuchukuliwa hatua za kisheria.