Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, amegoma kuhudhuria kesi yake ya uhaini akimtuhumu jaji anayesimamia kesi hiyo kuwa na upendeleo.
Besigye, aliyewahi kuwa daktari wa Rais Yoweri Museveni na mgombea wa nafasi ya urais mara nne nchini Uganda, anashikiliwa na mamlaka za kiusalama kwa tuhuma za uhaini dhidi ya serikali.
Ifahamike kuwa Besigye aliwekwa kizuizini pamoja na msaidizi wake Novemba 2024 katika nchi jirani ya Kenya na kurejea Uganda, ambapo wote wawili walishtakiwa kwa uhaini na makosa mengine awali katika Mahakama ya Kijeshi kabla ya kesi hiyo kuhamishiwa katika Mahakama ya Kiraia.
Imeelezwa kuwa Besigye alitakiwa kufika mahakamani jana Jumatatu kusikiliza kesi yake, iliyocheleweshwa kwa miezi kadhaa, lakini aligoma akimtaka jaji anayesimamia kesi hiyo, Emanuele Bugumu, kujiondoa.
Taarifa iliyotolewa na wakili wa Besigye, Eron Kiiza, imesema kuwa kiongozi huyo ameamua kususia kesi yake mpaka pale Mahakama itakapowasikiliza na kufanya uamuzi wa kumuondoa wakili anayesimamia kesi hiyo kwa sasa.
“Kesi ya Besigye na msaidizi wake, Obed Lutale, ilitakiwa kuanza kusikilizwa Jumatatu baada ya kuchelewa kwa miezi kadhaa, lakini washtakiwa wote waliamua kususia kusikilizwa kwa kesi hiyo baada ya hakimu, Emmanuel Baguma, kukataa kujitoa,” amesema Kiiza.
Amesema Baguma hana uwezo wa kutoa haki bila upendeleo kama inavyotakiwa na Katiba ya Uganda na tayari alishalithibitisha hilo kwa kumnyima dhamana Besigye kama msingi wa tuhuma hizo.
Ameongeza kuwa wakili huyo anashirikiana na mamlaka nyingine zinazofanya ukandamizaji dhidi yake, ikiwemo kumnyima dhamana na kuendelea kumpa mateso makali akiwa gerezani.
Ameitaja pia kesi ya Besigye na msaidizi wake, Obed Lutale, kuwa sehemu ya jitihada za Rais Museveni kufifisha na kudhoofisha wapinzani wenye nia ya kugombea kwenye uchaguzi mkuu ujao, akiwemo Bobi Wine.
Kwa upande wake, msemaji wa Mahakama, James Ereemye Mawanda, amekanusha madai hayo, akidai kuwa hakuna uhalali wa shutuma hizo za upendeleo huku akieleza kuwa malalamiko ya Besigye hayana mashiko.
Amesema Besigye na Lutale walichukua uamuzi wa kutofika mbele ya Jaji Baguma na wameona ni vema zaidi kuendelea kukaa gerezani.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kushindwa kwa watuhumiwa hao waliofunguliwa kesi dhidi ya Serikali ya Rais Museveni, ambaye pia ni mgombea wa kiti hicho katika uchaguzi ujao.
Elidaima Mangela, Sute Kamwelwe kwa msaada wa Mashirika ya Habari