Tanga. Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kurejesha heshima ya kihistoria ya mikoa ya Tanga na Morogoro kwa kuifanya kuwa maeneo tegemeo ya viwanda na uchumi wa Taifa, yatakayochochea ajira na maendeleo ya watu huku akiahidi petroli na dizeli kuuzwa chini ya Sh1,500.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika mwendelezo wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, zilizofanyika maeneo ya Mabanda ya Papa jijini Tanga leo Jumanne Septemba 2, 2025 Mwalimu amesema Serikali atakayounda kwa niaba ya Chaumma itawageuza wananchi wa Tanga na Morogoro kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya kweli.
“Serikali ninayoenda kuiunda na kuiongoza kwaniaba ya chama changu Tanga na Mkoa wa Morogoro itakuwa mikoa kitovu kwa viwanda na iwe tegemeo kwa nchi za Afrika Mashariki kwa uchumi,” amesema.
Amesema watakachokifanya ni kuboresha mipango kwakuwa mikoa hiyo ipo kimkakati na Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuonyesha dhamira wanaona wananchi mkineemeka itakuwa vigumu kuwatawala.
Amesema inawezekana wala haihitaji kwenda kuangalia kwenye vitabu, kuirudisha hadhi ya Mkoa wa Tanga iwe na viwanda kama ilivyokuwa zamani tofauti na sasa ilivyogeuka kuwa maghala, na vingine vimekufa.
Ameongeza kuwa haiwezekani Tanga ina reli, bandari, ardhi, mkonge na watu lukuki unashindwaje kufanya mageuzi ya kiuchumi tafsiri yake wanacheza.
“Serikali ya Chaumma haitakubali watu waendelee kuwa maskini ili hali kila fursa ipo, huku vijana wa Tanga wanateseka hakuna ajira, una ardhi, reli, bandari na mkonge hakuna ajira,” amesema Mwalimu.
Mwalimu amewataka wananchi wa Tanga kujiamini na Chaumma ikiingia madarakani inaenda kurejesha matumaini yao yanayoendelea kufifia kila uchwao na watafanya hivyo kuwaneemesha wananchi wote.
“Kiwanda moja wapo ninacho waahidi wananchi wa Tanga ni kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta yanayosafirishwa kutoka Uganda na Kenya kule eneo la Turkana wanamafuta hawatakuwa na ujanja lazima watakuja,” amesema.
Amesema baada ya kujengwa kiwanda hicho matarajio ya chama hicho mafuta ya dizeli na petroli yauzwe chini ya Sh1,500. Ahadi hiyo inatekelezwa tena kwa kiwango cha juu.
“Kama nchi imejenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, reli ya kisasa kwa gharama ya matrilioni ya fedha, sasa Mwalimu nasema alama nitakayoacha ni kuwajengea kiwanda cha kusafisha mafuta hapa Tanga wananchi waneemeke,” amesema
Mgombea huyo wa urais amesema jambo hilo linawezekana na watachimba mafuta ya ndani ili kuongeza uzalishaji huku akiwataka wananchi kuacha kucheza na mabadiliko anayohitaji kuyaleta.
“Naingia Ikulu sina mawaa, wala mihadi na mtu naingia Ikulu dhamira yangu ni kuwatumikia Watanzania kwa weledi kuhakikisha wanapata Maendeleo,” amesema.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa chama hicho kwa jimbo la Tanga mjini, Zainab Ashraf amesema ukosefu wa ajira kwa vijana ndio sababu iliyomfanya kugombea nafasi hiyo.
Amesema mkoa wa Tanga una fursa mbalimbali za kiuchumi ila wananchi wake wanashindwa kunuifaka nazo,nayo ni kutokana kukosekana wawekezaji ambao wangeweza kutoa ajira.