Tanga. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, atahakikisha vijana wa Kitanzania wanakuwa matajiri kupitia njia halali na endelevu.
Ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 2, 2025 wakati akihutubia wananchi wa kata za Maramba na Mapatano wilayani Mkinga mkoani Tanga katika mwendelezo wa kampeni zake alizozianza jana Jumatatu mkoani humo.
Mwalimu akijenga hoja za kushawishi umma kumpigia kura nyingi Oktoba 29 mwaka huu, amesema Serikali ya Chaumma itasimamia kwa nguvu zote sera zitakazowezesha vijana kujikwamua kiuchumi bila ubabaishaji wala ahadi hewa.
“Dhahabu zipo kila mahali, lakini wenyeji hawaoni faida yake. Sisi tukiingia Ikulu, tutaanza kwa kufanya mageuzi ya sheria na sera za biashara ndogondogo, kuhakikisha vijana wanalindwa, wanapewa mitaji na kufuatiliwa hadi wafanikiwe. Sitaki vijana waendelee kubabaika, nataka niwazalishe matajiri,” amesema.
Mwalimu pia amelaani kitendo cha wananchi kuondolewa kwenye maeneo yenye madini kwa visingizio vya uwekezaji, akisisitiza kuwa ardhi ni haki ya wananchi wa eneo husika hivyo chama hicho kikishika dola kitadhamini kwanza wenyeji.
“Haiwezekani madini yakigundulika, wenyeji waondolewe kiholela. Serikali ya Chaumma itahakikisha wamiliki wa ardhi wanalindwa na wanapata haki yao kabla ya kuondolewa,” ameongeza.
Katika hotuba yake, Mwalimu pia amesema Serikali ya CCM imeshindwa kutatua changamoto za msingi kama barabara na maji safi wilayani Mkinga, akidai kuwa wananchi wameachwa katika hali ya umasikini ili waendelee kutawaliwa kwa urahisi.
“Hawawezi kutengeneza barabara kwa sababu wanajua mkijengewa mtaamka kiuchumi. Mama mjamzito anabeba mizigo kama anaenda kuanza kidato cha kwanza Ghalanosia hii haikubaliki,” amesema kwa msisitizo.
Mwalimu pia ameahidi kutunga sheria zitakazolinda biashara ndogondogo na kuhakikisha kwamba mikopo ya halmashauri ya asilimia 10 inasimamiwa vizuri kwa manufaa ya vijana na wanawake.
“Vijana wana maarifa na wana uwezo mkubwa. Ila hawana mfumo wa kuwawezesha. Mikopo ya asilimia 10 ni kama mtego wa kisiasa. Tunahitaji mipango thabiti, si propaganda,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa katiba mpya itakayoweka msingi wa usawa, haki za wananchi na uwajibikaji wa viongozi, katika kushinikiza mambo wanayofikiria kupitia ilani yao yanafanyika.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Mkinga kupitia Chaumma, Rechael Sadick alitumia jukwaa hilo kueleza kuwa wilaya hiyo inahitaji ukombozi wa kweli baada ya miaka 60 ya umasikini na changamoto zisizopata suluhisho.
“Barabara mbovu, ajira hakuna, huduma za afya ni duni. Vijana wanalazimika kufanya kazi za manamba katika mashamba ya mkonge yasiyomilikiwa na wazawa. Hili ni janga la kiuchumi na kijamii,” amesema.
Rechael amewataka wananchi wa Mkinga kutumia nguvu ya sanduku la kura kuleta mabadiliko ya kweli, akisisitiza kuwa hakuna malaika atakayeshuka kutoka mbinguni kuwatetea ila wao wenyewe kupitia uamuzi sahihi wa kisiasa.
“Muda wa kupiga makofi umepita. Ninakwenda bungeni si kwa ushabiki, bali kujenga hoja, kusukuma maendeleo na kuhakikisha vijana wanashiriki katika kuijenga Tanzania mpya,” amehitimisha.