MZUMBE NA UNDP WAINGIA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

Farida Mangube, Morogoro

Katika jitihada za kuendeleza elimu ya juu, utafiti na ubunifu nchini, Chuo Kikuu Mzumbe kimesaini mkataba wa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)

Makubaliano hayo ambayo yanalenga kuimarisha mchango wa elimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) huku yakitoa fursa kwa vijana na watafiti nchini kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo yaliyofanyika Kampasi Kuu mkoani Morogoro, Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Rangi Mushi, amesema kuwa mkataba huo ni hatua muhimu kwa chuo hicho na taifa kwa ujumla katika kuimarisa tafiti.

“Makubaliano haya yatakuwa nguzo ya kuimarisha ubora wa tafiti, kuibua ubunifu na kuongeza mchango wa chuo chetu katika kutafuta suluhisho ya changamoto zinazolikabili taifa. Ni matarajio yetu kuwa ushirikiano huu utasaidia kupanua wigo wa elimu unayozingatia mahitaji ya jamii na maendeleo endelevu,” amesema Prof. Mushi.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara, amesema kuwa ushirikiano huo ni kielelezo tosha cha dhamira ya UNDP ya kushirikiana na taasisi za elimu ya juu katika kuharakisha maendeleo ya taifa.

“UNDP inatambua mchango wa vyuo vikuu katika kuibua mawazo mapya na suluhisho bunifu kwa changamoto za kijamii na kiuchumi. Kwa kushirikiana na chuo kikuu Mzumbe, tunaamini tutaweza kuimarisha uwezo wa vijana, kukuza tafiti zenye matokeo chanya na kuhakikisha tunachangia ipasavyo katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu nchini Tanzania,” amesema Komatsubara.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utekelezaji wake unatarajiwa kugusa maeneo mbalimbali ikiwemo kujenga uwezo wa watafiti wa ndani, kukuza teknolojia rafiki wa mazingira, kuendesha programu za kijamii kwa jamii za vijijini, pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na vijana.