UONGOZI wa Dodoma Jiji uko katika mazungumzo kumrejesha beki wake wa kati wa zamani, Ibrahim Ngecha baada ya Vedastus Masinde wa TMA ya Arusha aliyehitajika mwanzoni kudaiwa anakaribia kujiunga na kikosi cha Simba.
Masinde ni miongoni mwa mabeki waliohitajika na timu mbalimbali zikiwemo Singida Black na Dodoma Jiji, lakini inaelezwa yupo hatua za mwisho kwenda Simba ambayo itampeleka kwa mkopo JKT Tanzania.
Beki huyo inaelezwa ikiwa dili lake la kujiunga na Simba litakamilika ataungana JKT na mshambuliaji wa Simba, Valentino Mashaka ili wapate nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara.
Baada ya dili la Masinde kuonekana gumu kujiunga na Dodoma Jiji uongozi unafanya mazungumzo upya ya kumrejesha Ngecha ambaye hadi sasa kila kitu kinakwenda vizuri baina ya pande hizo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema benchi la ufundi litaamua lenyewe kama litaongeza wachezaji wengine wapya au la kutokana na upungufu litakaoona katika maandalizi yanayoendelea.
Ngecha mbali na kuichezea Dodoma Jiji, lakini timu nyingine alizochezea ni Fountain Gate na Mbeya Kwanza, huku kikosi hicho hadi sasa kikisajili nyota wengine wapya tisa, kwa ajili ya kuongeza nguvu katika msimu wa 2025-2026 wa Ligi Kuu Bara.
Nyota waliosajiliwa ni Miraji Abdallah ‘Zambo Jr’ (Coastal Union), Nelson Munganga na Andy Bikoko wote wakitokea Tabora United, sambamba na Faraji Kayanda na Castor Mhagama waliotoka KenGold ambayo imeshuka daraja na kwenda Championship.
Wengine ni Benno Ngassa aliyetoka katika kikosi cha maafande wa Tanzania Prisons, Edgar William na Dickson Ambundo wote wakisajiliwa kutokea Fountain Gate na aliyekuwa nyota wa timu hiyo Anuary Jabir aliyerejea tena akitokea Mtibwa Sugar.