Polisi, madereva wa treni mbaroni kwa tuhuma za wizi wa mbolea

Songwe. Watu saba wakiwamo askari wawili wa Jeshi la Polisi wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Songwe kwa tuhuma za wizi wa mbolea yenye thamani zaidi ya Sh45 milioni iliyokuwa ikisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda nchini Zambia.

Tukio la wizi huo linadaiwa kutokea Agosti 19 saa 7 hadi 8 usiku katika Kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani humo, ambapo watuhumiwa hao wanadaiwa walihusika kula njama.

Akizungumza leo Septemba 2, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Augustino Senga amesema watuhumiwa wakiwamo madereva wa treni wakishirikiana na wafanyabiashara wa mbolea kusimamisha treni hiyo 0139A mali ya Tazara.

Amesema katika tukio hilo, mifuko 534 ya mbolea hiyo aina ya Urea, yenye thamani ya zaidi ya Sh 45 mali ya kampuni ya Ocean Network ya nchini Zambia iliibwa.

“Treni hiyo ilisimamishwa eneo ambalo siyo kituo chake na kuanza kushusha mzigo, upelelezi ulianza haraka baada ya tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa saba,” amesema.
“Watuhumiwa hao wote ni wanaume, ambapo wawili ni askari wa Jeshi la Polisi (majina yamehifadhiwa kwa ajili ya upelelezi) waliokuwa wakisindikiza treni hiyo,” amesema Senga.

Kamanda huyo ameongeza kuwa baada ya doria, jeshi hilo lilifanikiwa kukamata mifuko 134 ya mbolea iliyokuwa imefichwa kijijini Iporoto kwenye nyumba ya mmoja wa watuhumiwa.

Amesema upelelezi wa kina kuhusu tukio hilo unaendelea ili kubaini na kuwakamata watuhumiwa wengine pamoja na vielelezo ikiwamo magari yaliyotumika kubeba mzigo huo.

Wakati huohuo, jeshi hilo linamshikilia Hussein Halili mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni fundi magari aliyekuwa kwenye harakati za kuvuka mpaka kupitia kituo jumuishi cha forodha Tunduma akiwa ameficha Dola za Marekani 160,000 ambazo ni takribani Sh400,000 milioni.

“Alibainika kuficha kiasi hicho ambazo ni zaidi ya Sh400 milioni ambazo alishindwa kutolea maelezo ya uhalali wake, akiwa ameficha kwenye koti lake kwa mgawanyo” amesema SACP huyo.

Amewataka wananchi mkoani humo kuacha kujihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwamo wizi, usaifirishaji haramu wa bidhaa na kuwataka watumishi wa Serikali kufanya kazi kwa maadili na uaminifu.