Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mkazi wa Kunduchi, Said Said (30) maarufu kama Popo, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka moja la kuzuia askari Polisi kufanyaka kazi yao.
Popo amefikishwa mahakamani hapo leo Jumanne Septemba 2, 2025 na kusomewa kesi ya jinai namba 21500 ya mwaka 2025.
Wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i amesomea shtaka lake, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Wakili Mbiling’i alidai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa lake Januari 2, 2025 eneo la Mbweni Wilaya Kinondoni.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa kwa nia ovu aliwazuia maofisa wawili wa Jeshi la Polisi wenye namba F.7025 Sajent Abdallah Idd na J.2591 PC Innocent, kufanya kazi yao.
Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake alikana kutenda kosa hilo na kuomba apewe dhamana.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wanaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali (PH).
Hakimu Mhini alitoa masharti manne ya dhamana kwa mshtakiwa huyo.
Alisema mshtakiwa atakuwa huru iwapo atakuwa na wadhamini wawili wenye barua kutoka Serikali za Mitaa na Kitambulisho cha Taifa (Nida).
Pia, wadhamini wao wawe ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na watasaini bondi ya Sh2milioni kila mmoja.
Hata hivyo mshtakiwa huyo ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kurudishwa rumande.
Hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 16 kwa ajili ya Serikali kumsomea hoja za awali mshtakiwa huyo.