RAIS MWINYI: AMANI CHACHU YA MAENDELEO

……….

Zanzibar | 02 Septemba 2025

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyopatikana katika uongozi wa Awamu ya Nane yamechangiwa na kudumu kwa amani, mshikamano na utulivu nchini.

Akizungumza na jopo la wahariri na waandishi wa habari Ikulu Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi alibainisha kuwa mazingira hayo yameiwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ufanisi.

📌 Mambo muhimu aliyoyasisitiza:

Ukusanyaji bora wa mapato na matumizi sahihi ya fedha za Serikali.

Uwezo wa Serikali kukopa na kuendesha miradi mikubwa, kutokana na nidhamu ya kifedha na utaratibu bora wa kulipa madeni.

Uanzishwaji wa akaunti maalum ya kulipia madeni (Debt Management Account) ambapo Serikali huweka dola milioni 15 kila mwezi (sawa na dola milioni 180 kwa mwaka).

Kuwekeza katika maendeleo ya wataalamu wa ndani na kuimarisha vyuo vya amali ili kuwajengea vijana stadi za kazi za kuajiriwa na kujiajiri.

🗳️ Kuhusu Uchaguzi Ujao

Rais Dkt. Mwinyi amewanasihi viongozi wa dini, wanasiasa na waandishi wa habari kuendelea kuhubiri amani na mshikamano kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Mkutano huo umefanyika baada ya jopo la wahariri na waandishi wa habari kutembelea miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika sekta mbalimbali Unguja na Pemba.