REKODI UTEKELEZAJI MIRADI SONGWE ZAMBEBA MGOMBEA URAIS CCM RAIS SAMIA SULUHU HASSAN,WANANCHI WANAMSUBIRI

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Songwe

WAKATI wa mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kufanya mkutano wake wa kampeni kesho Septemba 3,2025 mkoani Songwe ,wananchi wa Mkoa huo wanajivunia mafanikio makubwa waliyopata katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya mkutano katika Mkoa wa Songwe akiwa tayari mpaka sasa ameshafanya mkutano katika Mkoa wa Dar es Salaam , Morogoro na Dodoma.Katika mikutano yake maelfu ya wananchi wamekuwa wakijitokeza kumsikiliza.

Akizungumza leo Septemba 2,2025 kuhusu ujio wa Rais Samia katika Mkoa wa Songwe, Yusuph Rajabu ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM katika Mkoa huo amesema  katika miaka minne tangu Dk. Samia alipoingia madarakani, mkoa huo umepata mafanikio makubwa sekta ya afya kwa kujengwa hospitali ya rufaa ya mkoa.

Amesema kwamba zamanı watu walikuwa wakilazimika kwenda Mbeya kupata huduma za rufaa, lakini sasa huduma zote tunazipata hapa. “Mwaka 2020 tulikuwa na hospitali mbili za wilaya lakini sasa zipo tano. 

“Majengo matatu ya huduma za dharura katika hospitali ya rufaa yameanza kutoa huduma. Kwa upande wa zahanati mwaka 2020 zilikuwa 155 ila ndani ya miaka minne zimefikia 214 sawa na ongezeko la zahanati 55,” amesema.

Akieleza zaidi amesema mwaka 2020 watumishi wa afya katika mkoa huo walikuwa 570 lakini kwa miaka minne Dk. Samia ameongeza idadi ya watumishi kufikia 1,350 ikiwa ni ongezeko la watumishi 780.

Kuhusu nyumba za watumishi, ameeleza kwamba mwaka 2020 zilikuwa 922 ambapo sasa zimefikia nyumba 322.”Mimi ni mwalimu kitaaluma, katika elimu Rais Dk. Samia ameweka rekodi ya kipekee kwani idadi ya shule za msingi zimefikia 532 kutoka 455, shule za sekondari zimefikia 155 kutoka shule 120. Madarasa yalikuwa 3,600 lakini sasa yamefikia 4,272.”

Akieleza kuhusu ahadi ambazo mgombea Urais wa CCM , Rais Dk. Samia ameahidi kuzitekeleza ndani ya siku 100 pindi atakapochaguliwa, amesema ahadi ya ajira 500 kwa sekta ya afya na 7,000 kwa walimu wa hisabati na sayansi, zitatanua wigo wa ajira kwa vijana na kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika masomo hayo.

Pia amesema ahadi ya kutoa mtaji wa sh. bilioni 200 kwa wafanyabiashara wadogo, imewagusa wajasiriamali wa mkoa huo kwani wanaamini watakwenda kuongeza wigo wa mitaji yao kibiashara.

“Kuhusu suala la wahitimu wa mafunzo stadi kupata maeneo ya kuendeleza ujuzi wao, itawasaidia vijana kuendeleza ujuzi wao na kujiajiri kupitia taaluma walizozipata.

“Kwa Mkoa wa Songwe kwa kweli Mama Dk.Samia Suluhu Hassan hana deni bali sisi anatudai, maandalizi yamefanyika, wananchi wana matumaini makubwa hivyo tutampigia kura za heshima. 

“Mkoa wa Songwe katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwaka jana, tulishika nafasi ya nne kitaifa. Sasa kwa jambo hili la mama tunakwenda kushika nafasi ya kwanza kwa wingi wa kura za Rais.”

Baada ya Mkoa wa Songwe mgombea Urais Dk.Samia Suluhu Hassan ataingia katika Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kuendelea na mikutano yake ya kampeni kuomba kura kwa wananchi huku wengi wao wakiwa mashahidi wa yale ambayo yamefanyika katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wake.