Dkt. Magembe ametoa ufafanuzi huo leo Septemba 02, 2025 katika Ofisi za Wizara zilizozopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambapo amesema, mama huyo alifika hospitalini hapo Agosti 28, 2025 na kupata huduma ya kujifungua kwa njia ya upasuaji siku hiyo hiyo majira ya saa 1:40 usiku ambapo alipumzishwa tarehe 29 na tarehe 30, Agosti, 2025 aliruhusiwa na anaendelea vizuri.

Dkt. Magembe amesema video hiyo ilisambaa ikiwa na maelezo kuwa muuguzi huyo alikuwa anamtoa mzazi kondo la nyuma jambo ambalo sio kweli kwani kondo la nyuma hutolewa kipindi cha kujifungua kwa njia ya kawaida au kwa njia ya upasuaji, na tukio hilo halikutokea katika chumba cha kujifungilia au cha upasuaji bali ilikuwa ni wodini.
“Mama anayetolewa kondo kupitia via vya uzazi ni yule aliyejifungua kwa njia ya kawaida, mama huyu alijifungua kwa njia ya upasuaji na hivyo kondo lake lilitolewa akiwa chumba cha upasuaji na sio wodini,” amefafanua Dkt. Magembe

Dkt. Magembe amesema kuhusu chanzo cha Sakata hilo ni kuwa zilikuwepo tetesi za muuguzi huyo kuomba rushwa kwa wagonjwa na ndugu, ambao walieleza ndugu wa mama huyo waliombwa na muuguzi Shilingi 60,000.
“Kilichooneka ni mtego ambao uongozi wa Hospitali uliweka mara baada ya kupata taarifa za uwepo wa taarifa za muuguzi huyo kupokea rushwa huku ikisemekana alikuwa ametanguliziwa Shilingi 39,000 hivyo uongozi ukaweka mtego wa kumkamata akipokea kiasi kilichobaki cha Shilingi 21,000 hapo ndipo kulipozua taharuki, amesema Dkt. Magembe.

Kuhusu kuvaa Glovu Dkt. Magembe amesema kuwa ni sehemu ya kanuni na utaratibu wa watumishi wa afya wawapo katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku hususan pale mtumishi anapokuwa eneo la kazi, shabaha ikiwa ni kujilinda dhidi ya maradhi au kuambukiza wengine.
Akifafanua kuhusu hatua zilizofikiwa hadi hivi sasa juu ya mtumishi huyo, Dkt. Magembe amesema suala hilo lipo chini ya mamlaka zingine kama ilivyofafanuliwa kwenye taarifa iliyotolewa na mamlaka ya Halmashauri ya Kibondo.
Dkt. Magembe amewatoa hofu wananchi kuwa kwa sasa huduma za afya ya uzazi zimeimarika hivyo kupelekea vifo vya mama na mtoto kupungua kutoka vifo 556 mwaka 2021 hadi vifo 104 kati ya vizazi hai 100,000 mwaka 2024.