Shinyanga. Serikali imesema itatuma timu ya kamishna wa ardhi kwenda wilayani Kahama mkoani Shinyanga ili kuzitambua baadhi ya kaya zilizosahaulika wakati wa tathmini ya umilikishwaji wa ardhi katika eneo la zaidi ya ekari 300 za Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (Mwanva) FDC.
Wananchi hao ni wale waliosahaulika kwenye Takwimu zilizotolewa kwa Rais wa awamu ya tano hayati John Pombe Magufuli mwanzoni mwa mwaka 2021, alipotoa maelekezo ya wananchi waliodaiwa kuvamia eneo la zaidi ya ekari 300 za chuo, kumilikishwa kwa msamaha wa Rais huku chuo kikibaki na ekari 40.
Hata hivyo msamaha huo haukutekelezeka kutokana na kukosewa kwa takwimu zilizotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kwa Rais Hayati Magufuli, ambazo ziliwasahau baadhi ya watu waliokuwepo kabla ya msamaha huo.
Leo Septemba 2, 2025, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, ameielekeza halmashauri hiyo kuwaruhusu wananchi waliokuwepo awali, kufanya shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao, wakati ambapo Serikali inaendelea kushughulikia utatuazi wa wale waliosahaulika.
Akizungumza kwa njia ya simu kupitia kwa mkuu wa mkoa huo Mboni Mhita, wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Malunga, waziri Ndejembi amesema, “Wale ambao mlikuwepo kabla, jambo hili linafanyiwa kazi ili muweze kupata haki yenu, lakini kwa wale waliovamia baada ya msamaha, nasema hawana haki katika maeneo hayo, ni wale tu waliosahaulika kwenye takwimu za awali tu.”
“Huo ndio msimamo wa wizara, na muda si mrefu nitatuma timu ya kamishna ije kwa ajili ya kuwatambua hao ili tuweze kuona ni namna gani tunawapa miliki zao.”
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amesema “Niwape pole wale ambao mlipata changamoto kwa muda mrefu, lakini leo tumefika mwisho. Tunayafanya haya kwa maelekezo ya kiongozi wetu mkuu wa nchi Rais Samia Suluhu Hassan, tukazingatie maelekezo.”
Mstaafu wa Jeshi la Magereza, Gregory Kachemba amesema mgogoro huo ulimnyima usingizi kwani alimaliza mafao yake ya kustaafu kwa kujenga nyumba na kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo hata hivyo haikuendelea.
Amesema “Nilinunua kiwanja katika eneo hili kupitia kwa bwana ardhi likiwa limepimwa na nikapewa ofa, lakini mgogoro huu ulinitesa sana, sasa kupata suluhisho la mgogoro huu ni faraja kubwa kwangu.
Naye Shemsa Paschal ambaye ameishi kwenye eneo hilo tangu mwaka 2013, ameishukuru serikali kwa hatua hiyo kwani sasa itawarahisishia kuendeleza maeneo yao