Shambulio la Israel laua 17 Palestina

Gaza. Mashambulizi ya Jeshi la Israel yameua Wapalestina 17, wakiwemo watu sita waliokuwa wanakitafuta misaada, huku Israel ikieleza kuwa mashambulizi hayo yalilenga kundi la Hamas na waliofariki ilikuwa ni kwa sababu zingine.

Al Jazeera imeripoti kuwa, Israel ilitumia  vifaru  kulipua magari yaliyokuwa katika kitongoji cha Sheikh Radawan usiku wa kuamkia leo pia ilifanya mashambulizi ya anga kwa kutumia makombora.

Aidha wakazi wa eneo hilo wemesema, wanajeshi wa Israel pia walituma magari ya zamani ya kivita katika maeneo ya mashariki ya kitongoji hicho kilichojaa watu wengi, kisha kuyalipua kwa mbali na kuharibu nyumba kadhaa na kulazimu familia kuyakimbia makazi yao.

“Ulikuwa usiku wa kutisha, milipuko haikukoma na ndege zisizo na rubani ziliendelea  kufanya doria angani katika eneo hilo.

 Watu wengi waliacha nyumba zao wakihofia maisha yao, huku wengine wakiwa hawajui pa kwenda,” imelezwa.

Hata hivyo, Jeshi la Israel lilitoa taarifa likisema vikosi vyake vitaendelea kupambana na Hamas katika eneo lote na litaendelea kushambulia kambi kadhaa za kijeshi na kambi za nje ambazo zilitumika kufanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wake.

Wizara ya Afya ya Palestina imesema baadhi ya raia waliuawa kwa moto uliosababishwa na mashambulizi ya Israel.

Iliongeza kuwa watu tisa zaidi, wakiwemo watoto watatu, wamekufa kwa utapiamlo na njaa katika siku iliyopita, na kusababisha vifo kutokana na sababu hizo kufikia angalau 348, wakiwemo watoto 127.

Takwimu ambazo zinazopingwa na jeshi la Israel likisema kwa vifo hivyo vilitokana na sababu nyingine za kimatibabu.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesitisha  baraza lake la mawaziri la usalama siku ya Jumapili ili kujadili mashambulizi mapya na namna ya kuuteka mji wa Gaza, ambao ameutaja kuwa ngome ya Hamas.

Jeshi hilo pia Iimewaonya viongozi wake wa kisiasa kwamba mashambulizi yaliyopangwa katika mji wa Gaza yanaweza kuhatarisha mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas.
 
Hatua ambayo pia inapingwa na waandamanaji wa nchini Israel wakitaka  kusitishwa kwa vita na kuachiliwa kwa mateka walioshikiliwa na Hamas.

Elidaima Mangela UDOM kwa msaada wa Mashirika ya habari